Mkinga. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mkinga kupitia CCM, Twaha Mwakioja amewataka wananchi wa eneo hilo kumpa ridhaa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, ili aweze kushughulikia kero kubwa za muda mrefu za maji na barabara.
Akizungumza Jumapili Septemba 14, 2025, kwenye uzinduzi wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mapatano wilayani Mkinga, Mwakioja amesema kati ya vijiji 85 vya jimbo hilo, 37 vitanufaika na mradi mkubwa wa maji unaotarajiwa kuanza Oktoba kwa gharama ya Sh bilioni 35, na yeye atasimamia utekelezaji wake hadi kukamilika.
Ameongeza kuwa barabara ya Mkinga–Tanga imekuwa changamoto kubwa kwa muda mrefu, hivyo akipewa ridhaa atahakikisha inaboreshwa kwani tayari mipango ipo na kinachohitajika ni usimamizi wa karibu.
Aidha, ameahidi kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia rasilimali za bahari na misitu ili kuongeza kipato cha wananchi.
“Huduma za maji na barabara zitafungua uchumi wa wilaya ya Mkinga na kufanikisha maendeleo ya wananchi endapo nitachaguliwa kuwa mbunge,” amesema Mwakioja.
Akizindua kampeni hizo, aliyekuwa mgombea ubunge wa Tanga Mjini kupitia CCM kwenye mchakato wa ndani, Omar Ayoub amewahimiza wananchi kuendelea kuiamini CCM akibainisha kuwa chama hicho kimesimamisha wagombea kwenye kata 221 za mkoa wa Tanga na kimepeleka miradi mingi ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkinga, Abdallah Seif Singano, amewataka waliokosa nafasi ya kugombea kutovuruga mshikamano wa chama, akisema mshikamano ndio silaha ya ushindi.
Ameongeza kuwa ingawa upinzani upo kwenye kata 21 kati ya 22, CCM imedhamiria kushinda nafasi zote.
Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoa wa Tanga, Mwantumu Zodo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akiwahimiza wanawake kutumia nafasi yao kushawishi familia ili kuhakikisha wagombea wa CCM wanapata kura nyingi.
Pia, amebainisha kuwa Wilaya ya Mkinga inanufaika na ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe kitakachowezesha vijana kupata elimu na ajira.
Katika mkutano huo, mgombea udiwani Kata ya Mapatano, Marko Nakoli Mhanje, ameahidi kusimamia uboreshaji wa huduma za afya katika kata yake ili kuondoa changamoto zilizopo.