Mbeya. Mgombea Ubunge Mbeya mjini, Patrick Mwalunenge amesema iwapo atachaguliwa katika nafasi hiyo, atafunga baadhi ya barabara za jijini Mbeya nyakati za usiku ili vijana wafanye biashara kutengeneza uchumi.
Pia amesema atafunga taa baadhi ya mitaa katika Kata ya Iganzo na kujenga miundombinu ya barabara kwenye Kata hiyo, akisisitiza kuwa mkakati wake ni kuifanya Mbeya mjini kuwa kitovu cha utalii kutokana na milima iliyopo ya kipekee.
Akizungumza leo Septemba 15 katika mwendelezo wa kampeni zake, Mwalunenge amesema atalifungua jiji la Mbeya kiuchumi, akiahidi kuwa vijana lazima wafanye biashara na kujipatia kipato.
Amesema iwapo atachaguliwa pamoja na diwani wa Kata hiyo, Mwanjoka watashirikiana kujenga nyumba ya muuguzi katika kituo cha afya Iganzo, akiongeza katika uongozi wake hatakubali mtoto yeyote atakayekwama shule kwa changamoto yoyote.
“Samia alishatangaza elimu bure kuanzia msingi hadi kidato cha sita, nikishinda nafasi hii nitakuwa na utaratibu ofisini wa kutoa vifaa vya shule na chakula kwa watoto wasio na uwezo.
“Kama tunaweza kujenga masoko, tunashindwaje kuweka maeneo ya kulala au kupumzika watoto, hili la mama lishe anapika huku amebeba mtoto ni mateso, tutaweka utaratibu ili kila mtu afanye shughuli apate riziki,” amesema Mwalunenge.
Amesema ili kufikia malengo hayo, Mbeya Jiji itajengwa ukumbi wa kisasa wenye kufanyika vikao na mikutano kwa nchi za ukanda wa SADC, soko kubwa la Kimataifa hadhi ya Kariakoo ili wafanyabiashara wanaotoka nje kwenda Dar es Salaam waishie Mbeya.
Amewataka vijana jijini humo kujiandaa vyema kuchangamkia fursa hizo akieleza kuwa bodaboda na madereva bajaji lazima waheshimike kwani huduma zao zinachochea kukua kwa uchumi, akibainisha kuwa Mbeya lazima ifanane na majiji mengine.
“Sitakubali Mbeya Jiji kuona kina mama wanapanga bidhaa zao chini, kila mmoja atakuwa na meza ambazo tutazipa namba, tunataka mtu afanye kazi apate pesa, ninao uwezo katika biashara,” amesema mgombea huyo.
Ameongeza kuwa atafanya kazi usiku na mchana kupata maendeleo, “Tuondoe vumbi, uchafu na vichaka pori, tutashughulikia migogoro yoyote kabla ya kwenda mahakamani, kila nyumba iwe na mti ili kutunza na kulinda mazingira.”
Kwa upande wake aliyekuwa mtia nia ubunge, Sambwee Shitambala amesema kila mwana CCM anapaswa kulinda heshima na hadhi ya chama hicho kwa nguvu yake.
“Tunahitaji kuondoa makundi, tuwaunge mkono wagombea wetu ili Oktoba 29 tutiki mafiga matatu kuanzia diwani, mbunge na Rais, kila mmoja ajitahidi kulinda chama kwa heshima yote,” amesema Shitambala.
Mmoja wa kikundi cha wafanyabiashara wa mkaa, Nahumu Shamwela amesema changamoto kubwa ni gharama za nishati safi, namna ulipaji ushuru, adhabu kali za wanaokamatwa na mkaa na kunyang’anywa pikipiki.
“Tupo wafanya biashara 320, watu 120 wamekamatwa na kunyang’anywa na pikipiki zao, tunaomba utusaidie kukabiliana na changamoto hizi ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa uhuru kulipatia pato Taifa,” amesema Shamwela.
Naye Katibu wa CCM Mbeya mjini, Mohammed Mavallah amesema wagombea wote waliopitishwa na chama wanazo sifa, uwezo na uzoefu katika kuongoza.
“Tunaomba kura za ushindi na heshima kwa mgombea Urais Samia Suluhu Hassan, Mbunge Patrick Mwalunenge na madiwani wote akiwamo wa Kata ya Iganzo, Samwel Mwanjoka,” amesema Mavallah.