NAHODHA wa Kampala Queens, Shakirah Nankwanga amesema mashindano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ni fursa kwa wachezaji, akitamani kuacha rekodi.
Nankwanga mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na Kampala Queens akitokea Kawempe Muslim Ladies FC mwaka 2024 na akisaini mkataba wa miaka mitatu.
Katika msimu wake wa kwanza, alikuwa mchezaji muhimu akiisaidia timu hiyo kushinda taji la ligi, na alichaguliwa kwenye Kikosi Bora cha Wanawake cha FUFA cha Mwaka 2024.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, beki huyo alisema anatamani kuacha rekodi msimu huu kwani michuano hiyo imekuwa ikitoa wachezaji kwenda ligi mbalimbali kubwa.
“Kuwa nahodha wa timu ni heshima kubwa, lakini pia ni wajibu mzito. Natamani kuacha alama kusaidia timu kutwaa mataji, kuvunja rekodi na kuonyesha mfano mzuri kwa wachezaji wenzangu hasa vijana,” alisema Nankwanga na kuongeza:
“Binafsi, natamani kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kuichezea klabu hii. Hili ni jambo linalonihamasisha kila siku kujituma zaidi.”