NITASHIRIKIANA NA WANA-MUHEZA KUHAKIKISHA CHANGAMOTO ZINAONDOKA- MWANA FA

Na Mwandishi Wetu, Muheza

MGOMBEA ubunge Jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema ataendelea kushirikiana na wananchi wa wilaya ya Muheza kuhakikisha changamoto za Jimbo hilo linafanyiwa kazi.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Mkuzi, MwanaFA alisema kuwa changamoto zote zilizopo wilayani hapa anakwenda kuzifanyia kazi kwakuwa ni kipaumbele chake.

“Napenda niwahakikishie kuwa changamoto zote za wilaya ya Muheza nakwenda kuzifanyia kazi, hakuna jiwe ambalo litaachwa kugeuzwa…Changamoto zilizopo nakwenda kuzifanyia kazi na zitakuwa kipaumbele changu,” alisema mgombea huyo.

MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliwataka wananchi waende wakapige kura Oktoba 29 na wakawachague wagombea wa CCM kwakuwa katika kipindi cha miaka mitano wamefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alisema Muheza wamejipanga safari hii kuvunja rekodi ya watu waliojiandikisha kupiga kura watoke kwa idadi kubwa kwakuwa Jimbo hilo wameandikishwa watu 168,000.

“Ni uovu mkubwa kama umejiandikisha halafu hukwenda kupiga kura Oktoba 29, nawaomba amkeni asubuhi unamwamsha na jirani yako wale wapiga kura halali mnaenda kuchagua wagombea wa CCM,” alisema MwanaFA.

Alisema unapokwenda kupiga kura unakuwa na wajibu wa kuwauliza viongozi wao yale walitoaahidi na Kisha wakashindwa kutatekeleza kwa kuwa umekuwa na uhalali huo kwavile umepiga kura ya kuwachagua.

Akielezea kazi zilizofanyika katika kata ya Mkuzi ambayo imepokea jumla ya shilingi milioni 850 na kwa upande wa elimu ya msingi jumla ya sh. 248,436,056 ambazo zikipelekwa katika shule za msingi Mkuzi, Mafere na Mindu.

Alisema shule ya sekondari Mkuzi ilipata kiasi cha shilingi milioni 146.9 ambazo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, ujenzi wa maabara na matundu ya vyoo.

Hata hivyo, alisema shule nyingi za sekondari wilayani Muheza hazina mabweni ya wanafunzi wanaokaaa mbali waweze kulala akasema kwamba katika ilani ya uchaguzi jumla ya mabweni 15 yatajengwa.

Kwa upande wa afya alisema kuwa kata ya Mkuzi ilipata jumla ya shilingi milioni 280 ambazo zimepelekwa katika kituo cha afya Mkuzi kwa ajili ya kununulia vifaa tiba na majokofu ya kuhifadhia miili ya marehemu.

MwanaFA alisema katika wilaya ya Muheza wakati akiingia kuwa mbunge kulikuwa na kituo cha afya kimoja cha Mkuzi ambapo katika kipindi chake ameweza kufanikisha kupata vituo vya afya vingine ambazo ni za Ubwari ambayo hati katika eneo ilipojengwa haikuwepo na baada ya kupatikana kikapitishwa kuwa kituo cha afya na kuanza kupata mgao.

Kituo kingine cha afya kilichojengwa ni cha tarafa ya Bwembera kilichojengwa Kata ya Kwafungo, kingine ambacho tayari kimeingiziwa pesa kiasi cha shilingi milioni 645 ni kituo cha afya tarafa ya Amani. Kingine ni cha tarafa ya Ngomeni ambacho kinajengwa kata ya Misozwe kimeingiziwa shilingi milioni 250.

MwanaFA aliwaambia Wana Mkuzi kwanini anaomba kura na wanatakiwa kuichagua CCM ni kwasababu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameweza kutatua changamoto mbalimbali katika Jimbo hilo hivyo anatakiwa kupata kura za kishindo.

“Mimi nina kimbelembele cha kusemea mahitaji ya Wana Muheza lakini anayetoa fedha ni Dkt Samia Suluhu Hassan  hivyo mnatakiwa msipote kura hata moja katika wilaya yetu,” alisema. 

Akizungumza kuhusu maji katika kata hiyo alisema jumla ya shilingi milioni 175 ambazo zimetumika katika miradi mbalimbali katika vijiji vya Mafere, Mkuzi na Mindu.

“Kama tatizo la maji halitakaa liishe Muheza kwa shilingi bilioni 40 tulizopata katika mradi wa miji 28 ambao hapa Mkuzi mtapata, basi halitakaa liishe,” alisema Mbunge.

Mgeni rasmi katika mkutano huo Mjumbe wa halmashauri Kuu ya mkoa wa Tanga Faraha Mvumo alimkabidhi ilani mgombea udiwani wa kata hiyo Sharifa Kivugo na Mbunge huyo.

Aliwanadi wagombea hao akiwemo Mgombea Urais Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo alisema CCM Ina dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mwisho