Othman aahidi neema kwa watumishi Zanzibar

Zanzibar. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT–Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuunda Serikali, ataweka kima cha chini cha mshahara wa Sh1 milioni kwa watumishi wa umma.

Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT–Wazalendo, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza morali na ufanisi wa kazi kwa watumishi, huku akisisitiza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa kada za elimu na afya.

“Lazima tuimarishe uwezo wa kimaisha wa watumishi wetu. Ndiyo maana nasema mshahara wa chini hautapungua Sh1 milioni. Hili linawezekana, si propaganda za kampeni. Tumefanya mahesabu, tupeni ridhaa tulitekeleze,” amesema Othman.

Ameyasema hayo jana Jumapili Septemba 14, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake upande wa Unguja katika Uwanja wa Kibanda Maiti.

Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa ahadi hiyo, Othman amesema ana uzoefu wa uendeshaji wa masuala ya kifedha serikalini kwani alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Bodi ya Mapato Zanzibar.

“Ninaijua njia ya kukusanya mapato pasipo kumkamua mwananchi. Kuna fedha nyingi zinazotokana na mchango wetu kwenye Muungano, tutakwenda kuzidai ili Wazanzibari wanufaike,” amesema.

Amesisitiza kuwa huduma bora kwa wananchi haziwezi kupatikana bila watumishi wenye maisha yenye heshima na hali bora inayoongeza morali ya kazi.

Katika hotuba yake, Othman pia aliahidi kuboresha mazingira ya utendaji wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwemo KMKM (Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo) na JKU (Jeshi la Kujenga Uchumi).

Amesema vikosi hivyo vilianzishwa na waasisi wa Zanzibar kwa ajili ya kuilinda nchi na kuwahudumia wananchi, lakini kwa sasa vimekuwa vikikabiliwa na uhaba wa vifaa vya kisasa.

“Nimewahi kushuhudia hali halisi, mfano nilipokwenda Kisiwa cha Panza nikapanda ‘fiber’ nikaona hatari tuliyonayo. ACT–Wazalendo tunataka kurudisha heshima ya vikosi vyetu kwa kuwapatia nyenzo za kisasa, siyo kuwaambia wakapige wenzao,” amesema.

Ameongeza kuwa iwapo atashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Serikali yake itanunua vifaa vya kisasa kwa vikosi hivyo ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT–Wazalendo, Salim Biman amewaomba wananchi wa Zanzibar kuwapigia kura wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge, uwakilishi hadi urais, ili kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo ugumu wa maisha.