RAIS SAMIA AWALIPIA ADA YA MAFUNZO WANAWAKE WAJASIRIAMALI 3,000 WA DAR

:::::::

Mteule wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Elias Mahawanga, ameungana na kundi la Wanawake na Samia wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao wamehitimu mafunzo yao katika Chuo cha Veta Jijini Dar es Salaam Septemba,12 mwaka huu.

 Idadi ya Wanawake 405 ambao ni kundi la kwanza wamepata vyeti vyao baada ya kuhitimu mafunzo hayo na kuwa wanufaika wa fursa hii kati ya Wanawake 3,000 ambao wamekwishalipiwa ada.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kuwapongeza wahitimu hao Mahawanga ametoa shukrani za dhati na kumpongeza sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa fursa hiyo adhimu ya akina mama Wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

Amesema ufadhili huo umeleta chachu ya maendeleo kwa Wanawake Wajasiriamali kwani ilikuwa ni kiu yao ya muda mrefu sana kupata ufadhili huo wa masomo katika Chuo cha Veta kujiongezea ujuzi kwenye shughuli zao za kila siku, kupata fursa za kujiajiri na kuajiriwa, kuchangia maendeleo ya Taifa sambamba na kujiimarisha kiuchumi.

Vile vile Mahawanga amewapongeza sana timu nzima iliyohakikisha utaratibu mzuri unawekwa ili mafunzo haya kufanikiwa chini ya Mkurugenzi Mkuu wa Veta CPA Anthony Kasore, Mkuu wa Chuo cha Veta Dar es Salaam mhandisi Joseph Henry Mwanda, Mkurugenzi wa kanda Florence Kapinga, Walimu na Wafanyakazi wote, Katibu Mkuu wa Wanawake na Samia Taifa Hamida Mohamed sambamba na Mweyekiti wa kundi la Wanawake na Samia Mkoa wa Dar es Salaam Sophia Kinega kwa jitihada kubwa waliyoifanya kuhakikisha jambo hili zuri linawezekana.

 Mahawanga amesema fursa hii aliyoitoa, Rais niya kishujaa sana na imeandika historia mpya ya ukombozi wa Mwanamke kupitia elimu ya ufundi na ni ishara kwamba hakuna tena Mwanamke atakayebaki nyuma katika safari ya maendeleo ya Taifa letu kwani inaonyesha kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kutambua kwamba elimu ya ufundi ni nguzo ya maendeleo ya viwanda.

 Vilevile alisema fursa hiyo itapunguza changamoto za kifedha ambazo mara nyingi zimekuwa kikwazo kwa mabinti na akina mama wengi Wajasiriamali ndani ya Mkoa wetu wa Dar es Salaam.

Mahawanga amewasisitiza Wanawake wote 405 waliomaliza mafunzo yao wazingatie kuwa Mh. Rais ameshawapa fursa ya elimu sasa ni wakati wao kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi, wanavisajili na kuomba mikopo ya Halmashauri wakafanye kazi kwa vitendo kwa kutumia ujuzi walioupata na mitaji hiyo ambayo Serikali imekuwa ikitoa kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

 Kulikuwa na changamoto ya wajasiriamali wengi kukosa ubunifu wa biashara lakini sasa tayari mafunzo wameshapa hivyo tusimuangushe Mh. Rais iwe fursa hii iwe na tija ndani ya Taifa letu na Mkoa wetu.Mwisho Mahawanga aliwapongeza sana wahitimu kwani waliweza onyesha umahiri wao kwa kuandaa mabanda ya maonyesho ambayo walitengeneza bidhaa mbalimbali zilizotokana na mafunzo waliyoyapata kwani zilikuwa ni bidhaa bora naza viwango vya juu sana.