Dar es Salaam. Kasi ya ukuaji wa biashara Kariakoo imeibua tatizo jipya la usalama baada ya kuibuka kwa matukio ya moto yaliyohusishwa na wapangaji kuhamia katika majengo kabla ya kukamilika.
Ndani ya mwezi mmoja wa Agosti pekee, zimetokea ajali mbili za moto katika majengo yanayoendelea na ujenzi, huku kukiwa na wapangaji wanaoendelea na biashara zao.
Agosti 13, 2025 lililotokea tukio la moto saa 2 usiku katika moja ya majengo ya biashara Kariakoo maarufu Jengo la DDC Kariakoo.
Moto huo ambao chanzo chake hakikufahamika, ulianzia kwenye chumba cha masuala ya umeme na kusababisha taharuki kwa watu waliokuwepo eneo hilo wakiwepo wafanyabiashara.
Agosti 31, mwaka huu jengo lingine ambalo halijakamilika Mtaa wa Aggrey na Sikukuu lilishika moto na kusababisha chumba kimoja cha duka la jengo hilo kuungua.
Hivi karibuni, Mwananchi ilizungumza na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi ambaye alisema tukio la Agosti 13 lilikuwa kengele ya tahadhari kwa wote kuhakikisha majengo yanakidhi viwango vya usalama kabla ya kutumika.
“Ni kweli hakuna madhara yaliyotokea, lakini tukio hili limetufungua macho. Tunapaswa kuchukua hatua mapema kabla ya tukio kubwa linaloweza kuleta simanzi na hasara kutokea,” amesema Mushi.
Baada ya tukio la pili la kuungua kwa jengo hilo, Mushi alisema kutokana na mfululizo wa matukio ya moto wataitisha kikao cha wamiliki wa majengo ya Kariakoo, Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na watu wa Halmashauri kuona wanatokaje kwenye majanga hayo.
“Licha ya kuwa na kengele, lakini kuna haja ya kufanya kikao tuone tunatokaje hapa maana inaanza kidogo kidogo mwisho wa siku, yatatokea maafa makubwa, hivyo kikao hiki kitatupa tathimini ya tunatokaje katika eneo hili na nini kifanyike,” amesema Mushi.
Kutokana na matukio hayo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema ajali hizo zimeendelea kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara wanaoingia kwenye majengo ambayo hayajakamilika na kuendelea na shughuli zao.
Amesema wafanyabiashara wengi wanaingia kwenye majengo ya Kariakoo kukiwa bado miundombinu muhimu ikiwamo ya zimamoto haijakamilika katika baadhi ya majengo, jambo linaloongeza hatari.
“Kutokana na ajali hizo tunaendelea kufanya uchunguzi kujua chanzo na tutaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu majanga ya moto maana hakuna anayejua kesho moto utatokea kwenye jengo gani,” amesema Mabusi.
Mabusi amewataka wafanyabiashara na wapangishaji kuepuka kutumia majengo yasiyo salama, akisema ingawa changamoto ya upatikanaji wa maduka ipo, kuendelea kufanya biashara katika mazingira hayo kunaweza kuwasababishia hasara kubwa zaidi.
Wakati Mwabusi akiyasema hayo, Mei 5, 2025 katika uwasilishaji wa wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa Fedha 2025/2026, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema wizara hiyo inatunga sheria ya majengo kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya majengo nchini.
Mfanyabiashara wa nguo Mtaa wa Muhonda, Ali Abdul amesema ukosefu wa maeneo ya kudumu ya biashara umekuwa ukilazimisha wengi kukubali hatari ili mradi tu wapate nafasi ya kufanya biashara.
“Ukikosa duka Kariakoo, biashara yako inakufa. Wateja wanakuja huku kwa wingi, hivyo tunalazimika kuingia hata kama jengo bado lina matatizo. Kodi zenyewe ni kubwa, unalipa mapema kwa hofu ya kupoteza nafasi,” amesema Abdul.
Rose Mbilinyi, amesema wanaingia mapema kwa sababu ya shinikizo la kifedha, kwa sababu wanakuwa tayari wameshakopa fedha kwa ajili ya bidhaa na hawawezi kukaa bila kufungua maduka.
“Kuna wakati mtu unakopa benki au kwa mfanyabiashara mwingine. Ukichelewa kufungua, unazidi kudaiwa. Bora uingie mapema upate hata faida ndogo kuliko kukaa bila kufanya biashara,” amesema Rose.
Mhandisi wa umeme, Josephine Mutashobya amesema chanzo kikubwa cha moto ni nyaya kuunganishwa bila kufuata viwango vinavyokubalika.
“Majengo haya mengi yanapokimbiliwa na wapangaji, mara nyingi mafundi wanaajiriwa kwa haraka, na wamiliki wanataka umeme uweze kutumika mapema. Hivyo, nyaya huunganishwa kwa kutumia vifaa vya bei rahisi na hakuna ukaguzi wa kitaalamu kabla ya wapangaji kuanza shughuli,” amesema Josephine.
Amefafanua kuwa changamoto kubwa tatu ndizo zinazochangia ajali, ikiwamo kutumika kwa vifaa visivyokidhi viwango au kuunganisha bila mpangilio, hali inayosababisha nyaya kupitisha umeme kupita kiasi na kusababisha moto.
Pia, amesema baadhi ya majengo hayana mfumo wa kuondoa umeme wa dharura ardhini. Inapotokea hitilafu, umeme huzunguka ndani ya nyaya na moto huwaka.
Josephine amesema sheria inataka kila jengo lifanyiwe ukaguzi wa mwisho na wakaguzi wa umeme waliothibitishwa na mamlaka husika kabla ya kuunganishiwa huduma rasmi. Lakini mara nyingi umeme wa muda hutumika kinyume cha utaratibu.
“Hii ni sawa na kumruhusu dereva kuendesha gari bila breki kwa sababu tu injini inawasha. Ni hatari kubwa na matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona majengo kuungua moto,” amesema.
Aidha, amesema maeneo yenye msongamano mkubwa kama Kariakoo, huongeza hatari zaidi, kwa kuwa mara nyingi majengo hayo yanatumika kama maghala yenye shehena kubwa ya bidhaa zinazoshika moto haraka, kama vile nguo, viatu na plastiki.
“Moto ukianza kwenye jengo lisilo na wiring bora, unaweza kuenea kwa haraka na kuua watu au kuharibu mali za mabilioni ya shilingi ndani ya dakika chache,” amesema.
Baadhi ya makandarasi wanasema hali ya moto kujirudia katika majengo mapya Kariakoo inatokana zaidi na shinikizo la wamiliki wa majengo wanaotaka wapangaji waanze kuingia mapema.
Joram Mwaipopo, mkandarasi wa majengo amesema mara nyingi wanalazimika kumalizia sehemu ndogo tu ya jengo ili wapangaji waanze kutumia, huku mifumo muhimu ya usalama ikiwa bado haijakamilika.
“Mara nyingi tunashinikizwa tukamilishe sehemu ndogo ya jengo ili wapangaji waanze kuingia. Hata kama mifumo ya moto na hewa haijakamilika, wamiliki wanataka kodi ianze kuingia,” amesema Mwaipopo.
Alisema mikataba ya ujenzi haina kipengele cha kulinda wajenzi endapo mteja atataka kuharakisha mchakato kinyume cha kanuni. Hali hii huwafanya wajenzi kukubali shinikizo ili wasipoteze kazi na matokeo yake, majengo kutumika yakiwa hayajakamilika.
“Wajenzi tunakuwa tumebaki katikati ya biashara na taaluma. Kitaaluma tunajua jengo halijakamilika, lakini kibiashara mteja anakulipa na anakutaka umruhusu apangishe, hapo ndipo tunakubali kwa shingo upande,” amesema.
Mtaalamu wa mipango miji, Joyce Mgaya amesema tatizo kubwa si ukosefu wa sheria, bali utekelezaji wake.
Amebainisha kuwa katika maeneo yenye shughuli kubwa za kibiashara kama Kariakoo, wamiliki wa majengo wamekuwa wakikimbilia kupata kodi bila kuzingatia taratibu za ukaguzi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 majengo ya kibiashara na makazi hayapaswi kuanza kutumika kabla ya kukamilika na kufanyiwa ukaguzi wa mwisho.
Sheria hiyo inataka kila jengo lipate Cheti cha Kukamilika Ujenzi, kinachotolewa na mamlaka husika baada ya wahandisi na wakaguzi kuthibitisha usalama wa umeme, mifumo ya majitaka, njia za dharura na vifaa vya kuzimia moto.
“Sheria ipo wazi hakuna mtu anayeweza kuingia kwenye jengo kabla ya ukaguzi wa mwisho na kupata cheti cha kukamilika. Lakini Kariakoo wamiliki wanakimbilia kodi, na ukaguzi unakuwa dhaifu. Hii ndiyo sababu ajali za moto zinajirudia mara kwa mara,” alisema Joyce.
Aliongeza kuwa, udhaifu wa utekelezaji wa sheria unatoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki na wajenzi kupuuza taratibu, hali inayohatarisha maisha ya mamia ya wafanyabiashara na wateja wao.
“Kama mamlaka zingekuwa na msimamo mkali na kuzuia jengo lolote kutumika kabla ya kukamilika, tusingekuwa tunashuhudia biashara zikiteketea kwa moto kila mara. Ni lazima sasa ukaguzi uwe wa kweli, sio wa makaratasi pekee,” alisema Joyce.