Arusha. Serikali imesema itaanza kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu waajiri wote nchini watakaowazuia wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
Hayo yamesemwa leo Septemba 15, 2025 jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Zuhura Yunus wakati akifungua semina ya siku tano kwa waajiri na viongozi wa matawi ya chama cha wafanyakazi wa Serikali na afya Tanzania (Tughe).
Yunus amesema kuwa watumishi kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi ni haki yao ya kimsingi, hivyo kitendo cha baadhi ya waajiri kuwazuia ni ukiukwaji wa haki za utumishi.
“Nimesikia hapa baadhi ya waajiri wanawazuia watumishi wao kujiunga na hivi vyama wakati sheria inaeleza wazi hiyo ni haki yao, sasa niseme huu ni ukiukwaji wa haki za watumishi, na sisi Serikali kwa upande wetu hatutasita kumchukulia hatua za kisheria na kinidhamu mwajiri yoyote atakayebainika kufanya kosa hilo,” amesema.

Mbali na hilo amewataka waaajiri wote nchini kuzingatia utaratibu wa kuitisha vikao vya Baraza la Wafanyakazi ili kuyafanya yawe na tija kwa Taasisi.
“Lakini pia mjenge utamaduni wa kuwajengea uwezo watumishi wenu hasa mafunzo yanayowakutanisha na wawakilishi wa wafanyakazi na wa waajiri, maafisa utumishi, maafisa tawala na wanasheria wa taasisi kwani kwa kufanya hivi itakuwa ni mwarobaini wa kutibu na kuondoa migogoro mahala pa kazi,” amesema Yunus.
Mbali na kuondoa migogoro, Yunus amesema hiyo pia itasaidia watumishi kujua miongozo, sheria na kanuni zinazosimamia utumishi wao wa umma na masuala ya ajira lakini pia kuweka mahusiano mazuri kazini na kuongeza tija inayotarajiwa katika kuwahudumia wananchi.
Mbali na hilo, Yunus pia amewataka viongozi wa matawi ya Tughe kuwashauri ipasavyo waajiri wao ili kuondoa tabia ya ukiukaji wa sheria na kanuni zinazounda Mabaraza ya Wafanyakazi.
Awali Katibu mkuu wa Tughe, Hery Mkunda amesema kuwa semina hiyo yenye washiriki zaidi ya 800 kutoka Taasisi 300 za serikali watajifungia hapo kwa siku tano kuanzia septemba 15 hadi 18, 2025 kwa ajili ya kujifunza mada kuu sita katika uboreshaji wa majukumu yao kazini.
Amesema miongoni mwa mada watakazojadili na kujifunza ni pamoja na nafasi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidigitali katika kuimarisha afya na usalama kazini.
“Pia watajifunza taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma, usuluhishi na uamuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi dhidi ya waajiri,” amesema.
Mbali na hilo, Mkunda amesema washiriki hao watajua kazi na huduma zitolewazo na vyama vya wafanyakazi, lakini pia uendeshaji bora na mchango wa mabaraza ya wafanyakazi katika kukuza tija.
“Mada nyingine ni uhuru, umoja, demokrasia na utawala bora sehemu za kazi, lakini pia mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi.
“Kwa kutambua pia changamoto ya afya ya akili sehemu ya kazi tutajadili hilo kwa kina na ile dhana ya emotional intelligence na umuhimu wake kwa viongozi na wafanyakazi sehemu za kazi,” amesema.
Mwenyekiti wa Tughe Joel Kaminyoge, amesema malengo ya kuanzishwa kwa mafunzo hayo yanayowakutanisha waajiri na wafanyakazi ni kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa waajiri, watumishi na wanachama wa Tughe lakini pia kuimarisha mahusiano mema baina yao sehemu za kazi ili kupunguza migogoro.
“Malengo mengine ni kuimarisha utendaji kazi na utawala bora kwa waajiri na viongozi wa Tughe sehemu za kazi sambamba na kutangaza chama na shughuli zake pia kuimarisha utoaji wa huduma bora za chama kwa waajiri na wanachama” amesema.
“Pia tunalenga kukumbusha haki na wajibu wa wafanyakazi na waajiri sehemu za kazi na kuhamasisha ushirikishwaji wa Wafanyakazi sehemu za kazi”.

Mmoja wa washiriki Neema Swai amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea uwezo viongozi wa matawi hasa katika kupunguza migogoro mahala pa kazi.
Amewataka watumishi wenzake kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kazini katika kuleta tija ili kuwaongezea nguvu katika harakati mbalimbali za kudai haki zao.