Sheikh Ponda aomba ridhaa Temeke, akikumbushia sakata la Mtwara

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Temeke kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda, amewaomba wakazi wa Temeke kumchagua kuwa mbunge wao ili kuweza kuwakilisha kero zao bungeni, kama alivyowahi kufanya kwa wananchi wa Mtwara wakati wa mgogoro wa gesi na mambo yakawa sawa.

Sheikh Ponda amesema hayo leo Jumatatu Septemba 15 2025, alipokuwa akizindua kampeni za ubunge za chama hicho zilizofanyika Kata ya Tandika Devis kona relini jijini Dar es Salaam.

Katika kuwaomba huko kura, Sheikh Ponda amesema hataki ubunge ili kuwa maarufu au kupata fedha kwa kuwa, kazi za kuwatetea wananchi amezianza siku nyingi na kukumbushia alipowatetea wananchi wa Mtwara kipindi cha mgogoro wa gesi yao, huku wakiwa hawajui watakavyofaidika na hatua hiyo.


“Ukiangalia mimi sio mtu wa Mtwara ni wa Kigoma lakini niliwapambania watu wa huko hadi kuona haki inatendeka.

“Hivyo, nitakapopata ridhaa naamini nitakuwa mwakilishi mzuri wa kwenda kuwakilisha yale ambayo yametokana na wananchi wa Temeke,” amesema Sheikh Ponda.

Mgombea huyo amesema kwenda bungeni haendi kutafuta umaarufu wala fedha, bali ni kupata nafasi ya kuweza kukaa katika vikao vya mamlaka ili kuwatetea wananchi.

Ameongeza kuwa, hii ni kutokana na waliowapa mamlaka wamewageuka wananchi, hujali masilahi yao, kodi wanazolipa wanajinufaisha wao na familia zao.

“Leo hii bungeni mmesikia wanataka kujiongezea mafao wanapostaafu pamoja na wenza wao, wakati wananchi hospitali maiti za jamaa zao zinazuiwa kwa kukosa fedha, hospitali zimegeuka mahabusu kwa wafu kuzuiwa wanapokosa hela za kulipa baada ya kutibiwa, hii sio sawa tunahitaji mabadiliko,” amesema Sheikh Ponda.

Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Kata ya Tandika, Ramadhani Mbau aliwaambia wananchi wa Temeke kwamba, wamewapelekea Sheikh Ponda kwa kuwa ni mtu mpambanaji anajulikana hadi na watu wa kawaida.

“Oktoba tuhakikishe tunakwenda kupiga kura na tunamchagua Sheikh Ponda.”

Mgombea udiwani wa Kata ya Tandika, Musa Bakari amesema Dar es Salaam ina majimbo 12 ila ana uhakika kwa uchaguzi ambao chama umeufanya, Jimbo la Temeke linaenda kutangazwa la kwanza kuwa mbunge wake ni Sheikh Ponda.

Hata hivyo Bakari amesisitiza msimamo wa chama hicho kuwa, Oktoba 29, 2025 watakwenda kulinda kura.

“Tunasema siku ya kupiga kura tukikukamata na makaratasi ya kupiga kura feki utakuwa na kumbukumbu mbaya katika maisha yako, kama una mpango huo ni bora ukaahirisha mapema,” amesema mgombea huyo.

Mwenyekiti Jimbo la Temeke, Athuman Upindo, amewataka wakazi hao siku ya kwenda kupiga kura wakati wanatoka majumbani mwao waangalie hali ya vyumba vyao wanavyolala ili kwenda kufanya uamuzi sahihi.

“Jambo la muhimu wakati unakwenda kupiga kura, anza kuangalia unapotoka chumbani kwako.

“Kwa kuwa unapotoka chumba kina kila takataka kama stoo na wakati huohuo watoto wamelala chumba kimoja,” amesema.