Simbu afunguka, ataja  kilichompa ujasiri Tokyo

Bingwa wa dunia wa marathoni, Alphonce Simbu amefunguka kilichombeba katika mashindano hayo alfajiri ya kuamkia leo Septemba 15, 2025 jijini Tokyo Japan.

Simbu ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya 25 ya dunia nchini humo akitumia saa 2:09:48, muda sawa na aliotumia mshindi wa pili, Amanal Petros wa Ujerumani wakitofautiana na Simbu sekunde 0.03, huku Iliass Aouani wa Italia aliyetumia saa 2:09:53 akihitimisha tatu bora.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka Japan, Simbu aliyeongeza spidi mita kama 50 kabla ya kumaliza mbio, akitoka nyuma na kumpiku Petros ambaye wengi waliamini ndiye angeibuka kuwa bingwa,  amesema alitumia akili ya haraka kubadili upepo.

Mtanzania huyo ambaye hakuwa akitajwa kuwa miongoni mwa washindi tangu kuanza kwa mbio hizo, amesema hali ya hewa ya Tokyo ilimpa maarifa mapya ya kupambana. 

“Kuna joto kali, hivyo ikabidi nitumie mbinu ya kukimbia kwa tahadhari, lakini nisiachwe sana, kwani katika riadha katika mazingira ya hali ya hewa kama hii ya Tokyo, kifanya unachaji mapema (unaongoza muda wote) kuna mahali utafika itakuzidi.

“Hivyo, ningetumia nguvu  kubwa mwanzo ingekata mwishoni na hicho ndicho kilitokea kwa Waganda ambao walikaa mbele muda mrefu baadae wakafeli, katika hali ya hewa kama ile lazima uwe makini,” amesema Simbu.

Akizungumzia namna alivyoweza kutoka nyuma mita kama 50 na kumpita mpinzani wake hadi kutwaa medali hiyo, Simbu amesema alipoingia eneo la uwanjani kwa ajili ya kumaliza mbio, jambo alilolifikiria kwa haraka na baadae kuona analiweza ni kumpita aliyekuwa mbele yake.

“Niliona nina uwezo wa kupambana na huyu mtu, nikasema ngoja tukaribie mwisho kabisa ili nije msitukize, tukiwa tumekabiza mita chache sana, nilifanya  hivyo kwa kuwa nilikuwa na nguvu hiyo, alipogeuka kunitazama tayari tulikuwa sambamba.

“Yeye (Petros) alijaribu kujihami angalau aniwahi kwa kutanguliza mkono au chochote, lakini tayari nilimuwahi na mbinu yangu ikawa imefanikiwa kwa kumpita kwa sekunde 0.03, ambao ni muda kidogo sana, ni kama kivuli tu,” amesema.

Amesema baada ya mbio hiyo, hata mpinzani wake hakutarajia, japo alimpongeza  lakini muda wote alimuuliza imekuwaje?

“Hata yeye alishangaa, hadi sasa (saa 10 jioni au saa 4 usiku kwa Japan), haamini nini kilitokea, alijua anamaliza wa kwanza, wakati tunakwenda kwenye ceremony (hafla) ya medali tulikuwa naye, akanipongeza kwa mara nyingine, lakini bado haamini nini kimetokea,” amesema Simbu kwa furaha.

Katika mashindano hayo, yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa wa Japan, Tanzania iliwakilishwa pia na mwanariadha, Josephat Gisemo ambaye katikati ya mbio alipata majereha ya msuli na kujikongoja hadi kumaliza kilomita 42, lakini hakufanya vizuri.

Akizungumzia ushiriki wa Tanzania, Simbu amesema wakati mbio inaanza, hawakuwa katika orodha ya wanariadha waliokuwa wakitajwa kufanya vizuri.

“Nilizungumza na Gisemo, tukahamasishana tupambane hadi tone la mwisho, ndicho kilitokea, hata yeye licha ya kupata majeraha ya msuli, lakini hakukubali kuishia njiani, amekwenda hadi mwisho na kumaliza,” amesema Simbu.

*Mtaka, Bayi wamzungumzia*

Baada ya ushindi huo, Rais Samia Suluhu Hassan katika mtandao wake wa Instagram alimpongeza bingwa huyo, akibainisha ushindi wake ni sehemu ya historia ya taifa, akimtaka kuendelea kuiheshimisha bendera ya taifa.

Mbali na Rais Samia, aliyewahi kuwa rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka ameiambia Mwanaspoti kwamba moja ya vitu alivyotamani kuviona ni mafanikio ya mwisho ya nyota huyo.

“Nilipokuwa rais RT, ndicho kipindi ambacho Simbu alikuwa ameanza kujulikana kidogo kidogo, wakati huo nikiwa ni DC (mkuu wa wilaya) tunakwenda kuwahamasisha kambini Kilimanjaro nikiwa na kocha Francis (John sasa ni marehemu).

“Tulifanya vingi, ikiwamo kumsaidia ili apate ajira jeshini angalau apate income (kipato) ya uhakika ukizingatia riadha ni individual sport (mchezo binafsi), tulifanya hivyo kuhakikisha wachezaji wetu wanafikia malengo,” amesema.

Akifafanua hilo, Mtaka amesema aliuongoza msafara wa Kamati ya Utendaji ya RT (sasa SRT) kumuona Rais Jakaya Kikwete Ikulu wakati huo.

“Pamoja na mambo mengine, pia lengo lilikuwa kuomba zikitokea nafasi za majeshi wachezaji wa riadha nao wachukuliwe ili wapate income ya kuwawezesha kufanya mazoezi na ndicho kilitokea na hatimaye leo, Simbu amefanya kile tulichokitengenezea njia awali,” amesema Mtaka ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Amesema kikubwa ambacho watu wanatakiwa wajifunze, hakuna jambo la kuamka asubuhi ukalipata, akimtolea mfano Simbu ambaye amekuwa katika riadha kwa miaka 15, amekimbia mbio za ndani, Olimpiki mara kadhaa, Mumbai marathoni, London marathon na mbio nyingine nyingi zilizomkuza na kumjenga.

“Hakukata tamaa aliweka nia na bidii, na uwekezaji wa muda yote hayo ndiyo chanzo, nakumbuka wakati tunaingia RT Gidabuday (Wilhelim sasa ni marehemu) alisema atachoma vyeti vyake timu ikileta medali, lakini huwezi leo kesho unashinda, lazima kuwekeza.

“Tunajifunza kwa Simbu leo, katika miaka 15 ya uwekezaji wake, leo ameiletea nchi medali ya dhahabu ya dunia, naamini na wanariadha wengine watapata tu, kikubwa ni kuwekeza, kuna na nidhamu na bidii, wakimtanguliza Mwenyezi Mungu,” amesema Mtaka ambaye mwaka 2017 Simbu aliposhinda shaba ya dunia alimpa zawadi ya kiwanja cha barabarani, huko Singida na kumtaka ajenge kitu cha uwekezaji ambacho kitakuwa alama kwa mwanariadha huyo anayemtaja Mtaka kwamba hakuwa tu kiongozi bali Mentor wake.

Bingwa wa zamani wa dunia wa mbio ya mita 1500, Filbert Bayi amesema ushindi wa Simbu ni matokeo ya kutokuta tamaa.

“Ukiangalia katika zile mbio, Simbu hakuwa anapewa nafasi kabisa ya kufanya vizuri, hata alipoingia pale uwanjani kwa ajili ya kumaliza mbio, angekuwa ni mwanariadha mwingine angekubali medali ya pili, lakini yeye hakutaka hivyo.

“Alipambana kwa nguvu zote na matokeo tumeyaona, hiyo ndiyo tabia ya Simbu, katika mashindano makubwa na hata madogo, si mtu wa kukata tamaa, anapambana hadi dkika ya mwisho,” amesema Bayi akiungana na Watanzania wengine kumpongeza.

Kwa ushindi huo, Simbu anaondoka na kitita cha zaidi ya Sh 175 milioni kutoka kwa waandaaji, Shirikisho la Riadha la Dunia (WA).

Katika mashindano hayo, WA inatoa kitita cha dola 70000 kwa bingwa, dola 35,000 kwa mshindi wa pili na dola 22,000 kwa mshindi wa tatu katika michezo ya individuals wakati kwa team inatoa kitita cha dola 80,000 kwa bingwa, dola 40,000 kwa mshindi wa pili na dola 20,000 kwa mshindi wa tatu, zawadi zikitolewa hadi kwa washindi nane katika kila upande.

Rais wa SRT, Rogart John Stephen akizungumza na Mwanaspoti kutoka Tokyo, amesema ushindi wa Simbu ni mafanikio ya Watanzania.

Rogart ambaye amechaguliwa hivi karibuni kuongoza Shirikisho hilo akipokea kijiti kutoka kwa Silas Isangi amesema, Simbu amefungua njia kwa wanariadha Watanzania ambao wanaamini wataendeleza nyayo zake katika mashindano mengine ya kimataifa yajayo.