Singida Black Stars mabingwa wapya Kagame 

SINGIDA Black Stars imeweka historia kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Cecafa Kagame kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Al Hilal ya Sudan mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa leo Septemba 15, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ni Clatous Chama ambaye ameifanya Singida Black Stars kuweka historia hiyo kufuatia mabao mawili aliyofunga dakika ya 19 na 58 ikiwa ni mechi yake ya tatu tu tangu aanze kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Mtipa mkoani Singida akitokea Yanga. 

Singida Black Stars imeendeleza rekodi yake nzuri katika mashindano hayo kufuatia kupata ushindi wake wa wanne kati ya mechi tano ilizocheza tangu hatua ya makundi, hivyo kumaliza mashindano hayo ikiwa na wastani wa ushindi kwa asilimia 80. 

Katika siku 13 za ushiriki wao katika mashindano hayo makongwe zaidi kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Singida Black Stars ambayo ilikuwa kundi A, ilianza kwa kutoka suluhu dhidi ya Ethiopia Coffee kabla ya kuzichapa Polisi ya Kenya mabao 2-1 na Garde-Cotes bao 1-0.

Timu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi iliendeleza ubabe wake katika hatua ya nusu fainali kwa kuichapa KMC mabao 2-0. Chama alianza kuichezea Singida Black Stars katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Garde-Cotes ikiwa ni siku moja tu tangu ajiunge na wenzake akitokea kwao Zambia.

Mzambia huyo alianza kufanye yake katika mechi yake ya pili ambapo ilifunga bao moja wakati Singida Black Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC, hivyo amemaliza mashindano hayo akiwa kinara wa mabao kwa timu hiyo.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo ya fainali, Chama alisema; “Haikuwa rahisi, wapinzani walikuwa bora kuliko sisi, wenzetu wamecheza Ligi ya Mabingwa, tulijua tunatakiwa kuwaheshimu, hivyo tulifanya hivyo na kupata ushindi.”

Kwa upande wake, Khalid Aucho alisema: “Nina furaha kuwa sehemu ya mafanikio haya. Nimekuwa hapa kwa sababu mimi ni mchezaji ambaye napenda changamoto, mimi ni mchezaji mwenye kupenda kufanya vitu tofauti nipo hapa kuifanya Singida kuwa timu kubwa.”

Singida Black Stars ilianzishwa mwaka 2016 kwa jina la Ihefu SC. Katika misimu yake ya mwanzo, klabu hiyo ilikuwa ikipanda na kushuka kati ya Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu Tanzania Bara. Mwaka 2020 ilipanda kwa mara ya kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara na kushuka, kisha ikarejea tena mwaka 2022 baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza.

Mwishoni mwa mwaka 2023, klabu hiyo ilinunuliwa na mmiliki mpya, ndipo ilibadilishwa jina na kuanza rasmi kuitwa Singida Black Stars, sambamba na kuhamishiwa mkoani Singida kutoka Mbarali mkoani Mbeya.

Ubingwa huo, umeifanya Singida Black Stars kupewa zawadi ya Dola 30,000 (takribani Sh75 milioni) pamoja na medali za dhahabu, wakati mshindi wa pili, Al Hilal ikipata Dola 20,000 (takribani Sh50 milioni) na medali za fedha, huku mshindi wa tatu APR ikiambulia Dola 10,000 (takribani Sh24 milioni) na medali za shaba baada ya kuifunga KMC bao 1-0.