Straika Pamba alalamikiwa TFF | Mwanaspoti

BAADA ya Pamba Jiji kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Kagera Sugar, Peter Lwasa, raia wa Uganda taarifa mpya ni nyota huyo atafunguliwa mashtaka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji (TFF), kwa sababu ya kupinga agizo la waajiri wake.

Iko hivi. Kager iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu na kwenda Ligi ya Championship, ilifikia makubaliano ya kumtoa kwa mkopo wa msimu mzima nyota huyo kwa Mtibwa Sugar, ingawa dili hilo lilikufa baada ya mwenyewe kutokuwa tayari.

Baada ya nyota huyo kukataa kujiunga na Mtibwa kwa mkopo wa msimu mzima, uongozi wa Kagera umeweka ngumu na sasa unataka kwenda TFF kufungua mashtaka kwa ajili ya kuweka pingamizi la kuhakikisha Lwasa hatocheza Pamba Jiji msimu wa 2025-2026.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Mtibwa ndio inayopambana kuhakikisha nyota huyo dili la kwenda Pamba linakwama na kupewa ruhusa ya kumtumia, kama walivyokubaliana ili kumalizia mkataba wa mwaka mmoja uliobakia kikosini.

“Ni kweli tunatarajia kufungua shauri hilo TFF muda wowote kuanzia sasa kupinga usajili wake kwenda Pamba, anasisitiza mkataba umeisha baada ya timu kushuka, ila anasahau suala hilo halikuwa katika maandishi,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha, alisema ni kweli wamesikia uwepo wa taarifa hizo, ingawa wanachotambua nyota huyo ni halali yao, hivyo wanachosubiria ni kile kitakachotokea kwa sababu wamejipanga.

Nyota huyo aliyejiunga na Kagera Agosti 15, 2024 akitokea KCCA ya Uganda, alisaini mkataba wa miaka miwili, ila aliwataarifu viongozi wa kikosi hicho mwaka mmoja uliobakia umevunjika rasmi kwa sababu timu hiyo imeshuka daraja.

Nyota huyo aliyefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, amechezea URA na KCCA zote za Uganda, Sofapaka, Kariobangi Sharks na Gor Mahia za Kenya, huku akiitumikia pia timu ya Lubumbashi Sports ya DR Congo.