Dar es Salaam. Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imemtaka aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole kufika ofisini hapo kutoa maelezo au ushahidi kuhusiana na tuhuma anazozitoa kwa umma kupitia mitandao ya kijamii.
Polepole aliyejiuzulu nafasi yake Julai 13, 2025 kwa madai hawezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, hivyo ameamua kwa hiari yake kujiuzulu nafasi yake ya uongozi na utendaji serikalini.
Tangu wakati huo, amekuwa akiibua tuhuma mbalimbali dhidi ya Serikali na taasisi zake.
Sababu Polepole kuitwa polisi
Leo Jumatatu Septemba 15, 2025 Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, David Misime limesema limefungua jalada la uchunguzi na linaendelea kuchunguza tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa kada huyo wa CCM.
“Tuhuma ambazo ametoa na anaendelea kuzitoa kulingana na jinsi alivyozielezea zinaashiria uwepo wa makosa ya kijinai na kwa mujibu wa sheria zinahitaji ushahidi wa kuzithibitisha zitakapo wasilishwa mahakamani. Tuhuma hizo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii, baada ya kufungua jalada na kuanza uchunguzi, Jeshi la Polisi mbali na kukusanya ushahidi, limekuwa likifanya jitihada za kumpata ili aweze kutoa maelezo au ushahidi na vielelezo vitakavyo thibitisha tuhuma hizo ili kuwezesha hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na ndivyo utaratibu wa kisheria ulivyo” taarifa hiyo ya Polisi imeeleza.
Pia, jeshi hilo limemuelekeza Polepole aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoa maelezo yake au ushahidi kuhusiana na tuhuma hizo anazotoa kwa umma kupitia mitandao ya kijamii.