Watatu wafariki dunia kwa kuzama maporomoko ya Kipengele, wamo watoto wawili

Njombe. Watu watatu wakiwamo watoto wawili wamefariki dunia katika maporomoko ya maji ya hifadhi ya Mpanga Kipengele, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.

Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa limetokea katika hifadhi hiyo iliyopo kata ya Mfumbi.

“Hilo tukio nilikuwa silijui, lakini RCO hapa ndiyo ananiambia tukio hilo limetokea huko Mbarali,” amesema Banga.

Amesema tukio hilo limetokea jana Septemba 14, 2025,  saa 8.30 mchana katika maporomoko ya maji yaliyopo katika hifadhi hiyo iliyopo kata ya Mfumbi.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Michelle Mwasongwe (5) na Jannel Mwasongwe (4), watoto wa Bertha Nicodem, mtumishi wa Benki ya NMB, tawi la Makambako, na Lilian Mandali (31).

Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya watoto hao kushindwa kuyamudu maji waliyokuwa wakiogelea katika sherehe ya pamoja (Get Together) ya wafanyakazi wa NMB Makambako, Wanging’ombe na Makete.

Amesema baada ya watoto hao kuonekana wameshindwa kuyamudu maji hayo, ndipo Lilian alijaribu kuwaokoa, lakini naye akazama. Miili ya marehemu imeopolewa na kuhifadhiwa katika kituo cha afya cha Mbuyuni, wilayani Mbarali.

Hata hivyo, Meneja wa Benki ya NMB Mkoa wa Njombe, Anthony Grantany, alipotafutwa, amekataa kuzungumzia tukio hilo na kusema kuwa kuna wengine wenye mamlaka ya kuzungumzia.

“Hilo siwezi kuzungumzia kwani wapo ambao wana mamlaka ya kuzungumzia,” amesema Grantany.