Watoto wenye makengeza waitiwa matibabu Dodoma

Dodoma. Watoto 24 kati ya 10,000 wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 15 wana matatizo ya macho, ikiwemo ugonjwa wa mtoto wa jicho, huku asilimia 4.5 ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma wakikabiliwa na upofu.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, na daktari bingwa wa macho kwa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Dk Amon Mwakakonyole, alipozungumzia kambi maalumu ya vipimo na matibabu ya macho kwa watoto wa umri huo, iliyoanza leo.

Kambi hiyo inatarajia kuhitimishwa Septemba 30, 2025, na wanalenga kupokea watoto 1,000 kwa ajili ya vipimo vya uchunguzi na matibabu, ikiwemo upasuaji. Watakaostahili watagharamiwa na Serikali.

Dk Mwakakonyole amesema tatizo la mtoto wa jicho kwa watoto mara nyingi husababisha pia upofu kwa mhusika kama halitashughulikiwa mapema, ingawa mgonjwa akiwahi matibabu hupona kabisa.

Ametaja sababu nyingi zinazosababisha watoto kuwa na matatizo hayo, ikiwemo makengeza, mtoto wa jicho, maumivu kichwani, kutokwa machozi na matongongoro.

Amesema pia matumizi ya vifaa vya kielektroniki kwa watoto bila kuzingatia kanuni ni chanzo cha tatizo hilo.

“Watoto wakiwahi mapema tunaweza kutibu changamoto hizo, ikiwemo makengeza, upasuaji wa kumtoa mtoto wa jicho na kusaidia katika uoni hafifu. Kwa ujumla, tutawasaidia watoto kufikia ndoto zao na kuwaondolea wazazi changamoto,” amesema Dk Mwakakonyole.

Hata hivyo, daktari huyo amezungumzia ugonjwa wa macho (Trachoma) ambao uliweka mizizi katika mkoa wa Dodoma, zaidi wilaya ya Kongwa, kwamba hivi sasa haupo, kwani kilichokuwa kinatokea ni wingi wa vumbi na uhaba wa maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Henry Humba, amesema kambi hiyo ya wiki mbili itafanywa na madaktari wazoefu kutoka hospitalini hapo kwa kushirikiana na madaktari kutoka hospitali nyingine wenye wataalamu wabobezi.

Dk Humba ameeleza kuwa wanatarajia kupokea watoto wengi kutoka mikoa jirani na Dodoma, na kwamba wamejiandaa na kuwaandaa wataalamu wao kwa kazi hiyo, ambayo mwisho wake wanaiona itakuwa na mafanikio makubwa.

Daktari bingwa bobezi wa macho kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma, Japhet Boniface akisoma taarifa ya utafiti wa hali ya magonjwa ya macho Jijini Dodoma leo Septemba 15, 2025



Wakati huo huo, daktari bingwa bobezi wa macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Japhet Boniface, amesema asilimia 54 ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 wanakabiliwa na upofu unaotokana na mtoto wa jicho.

Dk Boniface ametoa kauli hiyo wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya tafiti katika Mradi wa Macho Yangu, unaotekelezwa na Shirika la Sightsavers Tanzania, uliofanyika mkoani Dodoma.

Mganga huyo ametaja kiini cha matatizo hayo ni shinikizo la macho, matatizo nyuma ya jicho, kovu kwenye kioo cha jicho, na ugonjwa wa kisukari, huku akiwataka watu kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Thomas Ruta, amesema tafiti hiyo itawasaidia kupeleka huduma ya macho hasa maeneo ya vijiji, ambako ndiko liliko tatizo zaidi, lakini akaeleza kuwa tatizo hilo linatibiwa kuanzia vituo vya afya hadi hospitali ya kanda.