Geita. Mbunge wa zamani wa Chato, Dk Merdad Kalemani, na Deusdedith Katwale, wameahidi kushirikiana na wabunge wateule wa majimbo hayo kuhakikisha ndoto ya hayati Rais John Magufuli ya kuifanya Chato kuwa mkoa inatimia.
Kalemani na Katwale, awatiania kugombea ubunge wa Chato Kusini na Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), lakini kura hazikutosha.
Machi 26, 2021, wakati wa mazishi ya Magufuli, wazee wa Wilaya ya Chato walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia Chato iwe mkoa, ili kukamilisha ahadi ya mtangulizi wake.
Hata hivyo, akiwa Chato Oktoba 14, 2021, kwenye kilele cha mbio za Mwenge, Rais Samia alisema Serikali inakamilisha vigezo vitakavyoruhusu Chato kuwa mkoa.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge Chato Kusini, mbali na kumuombea kura mgombea ubunge, Pascal Lutandula, wamesema uchaguzi ndani ya chama umemalizika na sasa ajenda iliyobaki ni kuendeleza maendeleo ya wananchi wa Chato.
Dk Kalemani amesema Magufuli ndiye mbunge wa kwanza wa Chato baada ya kuitoa kutoka Biharamulo, na njia bora ya kumuenzi ni kuhakikisha ndoto yake ya kuipandisha hadhi Chato kuwa mkoa inakamilika.
“Kwa sasa hakuna kundi la Kalemani, Lutandula wala Magembe. Tubaki wamoja na tuisogeze Chato mbele,” amesema Kalemani.
Kwa upande wake, Katwale amesema ndoto ya kuona Chato ikawa mkoa lazima ibaki kuwa ajenda ya pamoja. Amesema licha ya kutoshiriki tena bungeni, atabaki kushirikiana na wabunge watakaochaguliwa kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Ameongeza kuwa changamoto za barabara, maji na umeme bado ni kikwazo kwa wananchi, na kuwataka wagombea hao kuhakikisha wanabeba changamoto hizo bungeni ili ndoto ya maendeleo ya Chato iweze kutimia.
“Niwaombe sana wana CCM ambao mlikua na makundi, sasa myasahau na muungane katika kampeni kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo kwenye kura za Urais, Ubunge na Udiwani,” amesisitiza Katwale.
Mgombea ubunge wa Chato Kaskazini amesema endapo atachaguliwa, ndoto na utabiri uliotabiriwa na hayati Magufuli ya Wilaya ya Chato kuwa mkoa na makao makuu kubaki Chato, itatimia.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Chato Kusini, Pascal Lutandula, ameahidi iwapo atachaguliwa atashughulikia changamoto za stendi, wakulima na soko, huku akisema Buseresere, eneo maarufu la biashara, litakuwa ‘Dubai ndogo’ kutokana na uwekezaji wa taa na miundombinu mipya.
Lutandula amewataka wananchi kutoa kura zote kwa CCM kwa kuchagua mafiga matatu ili waweze kuleta maendeleo.
Akizindua kampeni hizo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Gervas Evarist, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura, ili chama hicho kiweze kushinda ngazi zote.
“CCM imefanya kazi kubwa Chato. Kata 19 kati ya 23 zimepita bila kupingwa, hii ni ishara ya mshikamano. Msikubali kura za hapana kuwa nyingi. Tujitokeze kupiga kura ili kukiwezesha chama kuendelea kushika dola,” amesema Evarist.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule 26, zahanati 14, vituo vya afya 6, hospitali, soko na kituo cha mabasi, vimejengwa.