AZZA HILLAL AMUOMBEA KURA AHMED SALUM, DR. SAMIA


Mgombea Ubunge Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Jimbo la Solwa

Mgombea Ubunge Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akiomba kura kwa ajili ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ahmed Salum, Madiwani wa CCM na yeye mwenyewe akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Jimbo la Solwa

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MGOMBEA wa Ubunge wa Jimbo jipya la Itwangi Azza Hillal Hamad,ametinga Jimbo la Solwa kushiriki uzinduzi wa kampeni za CCM, na kuwaomba wananchi kura za ndiyo kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Ally Salum na madiwani wote wa CCM.

Uzinduzi wa kampeni hizo umefanyika leo Septemba 15,2025 katika Kata ya Lyamidati,ukihudhuriwa na wananchi, wanaCCM na wagombea udiwani.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Azza amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kwamba ndani ya miaka yake mitano amefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi likiwamo na jimbo la Itwangi ambapo miradi mingi imetekelezwa na kila kijiji kimefikiwa.

Amesema Jimbo la Solwa kabla ya kugawanywa lilikuwa na kata 26, na miradi ya maendeleo imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, hivyo wananchi wanapaswa kumpa fadhila Rais Samia kwa kumpigia kura nyingi Oktoba 29, ili aendelee kuliletea taifa maendeleo.

Amempongea pia Ahmed,kwa kazi ambayo ameifanya ya kulihudumia Jimbo zima la Solwa kabla ya kugawanywa, ambapo ametekeleza miradi mingi ya maendeleo,na kwamba anastahili kupewa mitano tena sababu ni kiongozi mchapakazi na mpenda maendeleo.

“Naomba nipige magoti kwa heshima yenu kumuombea kura Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,kaka yangu Ahmed Salum na Madiwani wote wa CCM,”amesema Azza.


Azza,amesema maendeleo ni hatua kwa hatua, na kwamba pale ambapo ameishia Ahmed kwa upande wa Jimbo la Itwangi, kuwa anawaomba wananchi wa Itwangi wampatie ridhaa ya kuwa Mbunge wao ili aendeleze guruduma la maendeleo.

Naye Ahmed, amemuombea kura Azza kwa wananchi wa Jimbo la Itwangi, ili awe Mbunge wao, na kwamba wakipata ridhaa ya wananchi,watafanya kazi kwa pamoja na kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Shinyanga Vijijini.

“Tukiwa Bungeni nitafanya kazi kwa kushirikiana na Dada yangu Azza la kwake la kwangu, na langu la kwake lengo ni kuchapa kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi,”amesema Ahmed.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela, naye alimwagia sifa Ahmed kwamba licha ya Jimbo hilo la Solwa awali kuwa kubwa lakini alifanya kazi kwa bidii ya kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo.

Jimbo la Solwa limesha gawanya na kuwa na majimbo mawili ya Uchaguzi, likiwamo Jimbo la Solwa lenyewe ambalo lina Kata 12, na Jimbo Jipya la Itwangi lenye Kata 14.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Solwa.



Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Solwa.


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akinadi sera na ilani ya CCM kwa wananchi.