Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema wananchi wa Zanzibar wanapenda amani, maendeleo na sio porojo.
Ametoa kauli hiyo leo Septemba 16, 2025 wakati akizungumza na wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali wa Uzini katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kampeni za chama hicho, na kwamba ndio wenye uwezo pekee kutekeleza mambo hayo.
“Ukiwauliza leo Wazanzibari mnataka nini, watakwambia amani na maendeleo. Na wenye kuleta hivyo vitu ni CCM na sio wengine, kwa hiyo mkitaka vitu hivyo viendelee kichague Chama cha Mapinduzi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema CCM imethibitisha kwamba ina uwezo wa kulinda amani na kuleta maendeleo, iwapo kuna mtu anataka yaendelee basi wasifanye makosa kuchagua chama kingine kwani uwezo huo hawana.
Amesema wakati wanaingia madarakani mwaka 2020 kulikuwa na mifarakano mikubwa baina ya Wazanzibari kiasi cha kushindwa hata kuswali msikiti mmoja kisa siasa, lakini wamehakikisha wanakomesha jambo hilo.
“Kwa sasa hakuna ukabila, hakuna upendeleo katika ajira na utoaji huduma, tunakuombeni endeleeni kukiunga mkono CCM ili tulete makubwa zaidi,” amesema
Amesema iwapo wakichaguliwa tena wataweka mkazo kwa wakulima na wajasiriamali wapate vifaa, mazingira mazuri ya kulima na kuendeshea biashara zao.
Amesema wametoa Sh96 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali hivyo wakirejea madarakani watatoa zaidi ya mara mbili ya kiasi hicho kwa mkopo isiyokuwa na riba.
Dk Mwinyi, amesema pia kuna tatizo kwa wafugaji ambapo watawatafutia soko la maziwa huku wafugaji wa kuku wakiwekewa mazingira mazuri ya kuimarisha soko la ndani kwa kuthibiti bidhaa kutoka nje.
“Tutahakikisha tunajipanga kuimarisha kilimo na ufugaji kwa kutoa vipaumbele kwao,” amesema.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema hatua ya kukutana na makundi hayo ni kujenga imani na mshikamano.
“Ukichagua CCM ndio utakuwa umechagua maendeleo na Dk Mwinyi ndio anaweza, maana nia anayo, uwezo anao na uthubutu anao,” amesema Dimwa.