KCB EAST AFRICA GOLF TOUR KUUNGURUMA LUGALO GOLF CLUB JUMAMOSI HII.

::::::::::


Mashindano ya mchezo wa gofu ya ‘KCB East Africa Golf Tour’ kuanza rasmi
Tanzania Jumamosi, tarehe 20 Septemba 2025, katika uwanja maarufu wa Lugalo
Golf Club, jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya wachezaji 200 wa gofu wanatarajiwa kushiriki, wakichuana kupata nafasi
ya kuwakilisha taifa kwenye fainali itakayofanyika Kenya mwishoni mwa mwaka
huu.

Fainali hiyo itajumuisha timu kutoka nchi tano za Afrika Mashariki kutoka
Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kila moja ikiwa na wachezaji wanne,
wakishindania zawadi ya shilingi milioni 1 za Kenya (sawa na TZS milioni 20),
fedha zitakazotumika kusaidia miradi ya uendelevu itakayopendekezwa na klabu
husika.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza mashindano hayo,
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Biashara wa Kanda wa KCB Group na Mkurugenzi
Mtendaji wa KCB Bank Tanzania, Gabriel Lekundayo alisema;

“Huu ni mwaka wa pili sasa tunaandaa mashindano haya makubwa katika ukanda wa
Afrika Mashariki. Tuna imani kubwa kuwa timu ya Tanzania itafanya vizuri katika
fainali na kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa,” alisema.

Mashindano haya yanatarajiwa si tu kuibua mabingwa wa kitaifa, bali pia
kuchochea mshikamano wa kikanda, kuimarisha ushirikiano wa mataifa jirani, na
kuendeleza ujumbe wa uhifadhi wa mazingira kupitia michezo.