KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025 ,MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI AVIFUNDA VYAMA VYA SIASA HANDENI

 

Na; Mwandishi Wetu – Handeni

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imevitaka vyama vyote vya siasa katika Wilaya ya Handeni kuhakikisha vinazingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi na kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika kikao kazi na wawakilishi wa vyama vya siasa katika Wilaya ya Handeni, Bi. Edna Assey kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa alisema kuwa jukumu la vyama vya siasa ni kuhakikisha vinashiriki uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha uhalali wa mchakato mzima.

“Vyama vya siasa haviruhusiwi kujihusisha na vitendo vya rushwa kama kutoa fedha, mikopo, zawadi au hata ahadi za vyeo kwa lengo la kushawishi wapiga kura. Kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinaweza kupelekea hatua kali za kisheria kuchukuliwa,” alisema Bi. Edna

Aidha, aliwakumbusha viongozi wa vyama kuzingatia haki na wajibu wao wakati wa kampeni, ikiwemo kuendesha kampeni za kistaarabu, kuheshimiana na kuepuka kutumia lugha za matusi, kejeli, uchochezi au vitisho dhidi ya vyama vingine.

Ofisi ya Msajili imeeleza kuwa uchaguzi ni zoezi la kitaifa linalohusu mustakabali wa taifa lote, hivyo vyama vyote vinapaswa kushiriki kwa kuonyesha mfano bora wa uongozi unaojali maslahi mapana ya wananchi na taifa.

Bi. Edna Assey alisisitiza kuwa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa kutasaidia kujenga mshikamano wa kitaifa, kuimarisha demokrasia na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pia imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kutumia haki ya kupiga kura na kufanya maamuzi kwa uhuru bila kushawishiwa kwa rushwa au vitisho. Wananchi wamehimizwa kutanguliza amani na mshikamano na wa kitaifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.