MSHAMBULIAJI mpya wa JKT Tanzania, Valentino Mashaka amesema anajipanga kuhakikisha huduma yake inaifaa timu hiyo kwa msimu wa 2025/26 unaotarajia kuanza Septemba 17.
JKT Tz itaanza mechi yake ya kwanza ugenini dhidi ya Mashujaa itakayopigwa Septemba 18, jambo ambalo Mashaka alisema anatamani kuanza na mguu wa neema wa kufunga bao, ili ndoto zake kuwa na nguvu.
“Natamani msimu huu kwangu nitajwe katika top3 ya wafungaji, baada ya msimu uliyopita kumaliza na mabao mawili pekee, kutokana na nafasi ndogo niliyokuwa napata ya kucheza,” alisema Mashaka na kuongeza;
“Nafurahia kujiunga na timu ya JKT Tanzania, akili yangu kwa sasa naihamishia katika kazi, itakayonitambulisha zaidi kwa mashabiki kukiona kipaji changu kwa ukubwa zaidi.”
Alisema yapo mambo mengi aliyojifunza Simba chini ya kocha Fadlu Davids na wachezaji aliyokuwa anashindana nao katika nafasi anayocheza.
“Ni muda sahihi wa kuyafanyia kazi niliyojifunza Simba kutoka kwa wachezaji wa ndani na nje, nafahamu ili uwe mchezaji mkubwa kitu gani napaswa kukizingatia,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema:”Mashaka ni mshambuliaji mzuri najua alikosa nafasi Simba, kikubwa ni utayari wake naamini atakuwa kati ya wachezaji ambao watatajwa kwa kufanya makubwa.”