Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameigomea Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili, kwa madai ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kufukuzwa mahakamani.
Lissu ametoa madai hayo leo Jumanne Septemba 16, 2025 kabla ya kuanza usikilizwaji wa sababu ya pili ya pingamizi lake la kupinga uhalali wa Mahakama hiyo kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.
Hivyo ameiomba Mahakama hiyo itoe amri ya ahirisho mpaka wafuasi wake hao watakaporuhusiwa kuingia katika ukumbi wa Mahakama inayosikilizwa kesi hiyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa ndani ya chumba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 16, 2025.
Hoja na maombi hayo ya Lissu yamepingwa vikali na Jamhuri ikisema kuwa madai ya wafuasi kufukuzwa mahakamani (ambayo hata hivyo Jamhuri imeyapinga), si sababu ya msingi ya ahirisho la kesi, badala yake mshtakiwa atakuwa amegoma kuendelea na kesi.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote imeahirisha kesi hiyo kwa muda wa saa moja kwa ajili ya kuandaa uamuzi na maelekezo ya namna ya kuendelea.
Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-

Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa katika majukumu ya kuimarisha ulinzi kwenye viunga vya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 16, 2025.
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Septemba 8, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.
Hata hivyo Lissu aliibua pingamizi akiomba Mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iitupie mbali akitoa sababu mbili, ubatili wa hati ya mashtaka na mamlaka ya mahakama, ambayo mahakama hiyo jana Jumatatu, Septemba 15, 2025, imeikataa.
Baada ya Mahakama kulikataa sababu hiyo ndipo Lissu akaendelea na sababu hii ya pili ya pingamizi lake, yaani ubatili wa hati ya mashtaka, aliyoianza jana.
Leo baada ya majaji kuingia tu mahakamani baadhi ya wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa ndani ya ukumbi wa Mahakama wamenyanyuka kwa pamoja na kutoka nje ya ukumbi huo.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa ndani ya chumba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 16, 2025.
Baada ya utambulisho wa pande zote ndipo Lissu akaibua madai hayo ya kufukuzwa kwa wafuasi wake na kuomba ahirisho hilo mpaka watakaporuhusiwa kuingia
Saa 3:27 asubuhi Jopo la majaji watatu liliingia mahakamani na baada ya kuingia wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga akaieleza Mahakama kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.
Hata hivyo Lissu alivyopewa nafasi ya kuieleza Mahakama iwapo yupo tayari kuendelea alidai kuwa yupo tayari lakini kuna jambo anataka kulieleza.
“Waheshimiwa majaji, katika mazingira ya kawaida, nitasema nipo tayari, watu wametolewa ndani kwa maagizo ya ZCO( Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam), wanakatazwa kuhudhuria mashauri haya, hii haikubaliki na mshtakiwa” amedai Lissu na kuongeza.
“Hii ni Mahakama ya wazi na sio ya kijeshi, hii ni mahakama ya kiraia na ni Mahakama Kuu na watu wenye mamlaka ya kufanya chochote ni majaji na sio ZCO ,RPC wala Samia” amedai Lissu

Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa katika majukumu ya kuimarisha ulinzi kwenye viunga vya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Septemba 16, 2025.
Ameendelea kudai kuwa Mahakama Kuu ndio pekee na kwamba hakuna kesi kubwa kama hiyo na shauri hilo lina wajibu mkubwa wa kufuatiliwa.
“Kesi hii inafuatiliwa kwa ukubwa na watu wa nje, vyombo vya habari, sasa inawezekanaje polisi wanatoa amri mbele ya majaji.
“Sisi leo karne ya 21 polisi wanatoa watu mahakamani mbele ya majaji na majaji mkiruhusu hii itakuwa mahakama ya giza” amedai.
Lissu ameomba kabla ya kuendelea na shauri lake, mahakama hiyo itoe amri ili watu waliotolewa ndani ya mahakama ya wazi namba moja warudishwe.
Pia ameomba mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi watu hao waliotolewa nje watakaporudishwa ndani ya mahakama hiyo.
Baada ya kumaliza kuwasilisha taarifa hiyo, Serikali ilipewa nafasi ya kujibu hoja zilizotolewa na Lissu.
Akijibu hoja hizo, Katuga amepinga vikali kesi hiyo kuahirishwa akieleza sababu zilizotolewa na mshtakiwa hazina mashiko.
Katuga amedai kuahirishwa kwa mwenendo wa kesi iliyopo Mahakama Kuu, kuna sheria na kanuni lazima na alidai kifungu 302 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023, ambacho kinatoa mamlaka ya kuahirisha kesi hiyo.
“Tunajiuliza kutokuwepo watu ndani ya ukumbi wa mahakama ya wazi, ni msingi wa kuahirisha kesi hii? Na wala hakuna amri ya mahakama kuwazuia, tunajiuliza ni sababu ya kushindwa kuendelea na kesi hii” amehoji Katuga na kuendelea.
“Waheshimiwa majaji, Lissu ameiambia mahakama watu wameondolewa, sisi upande wa Jamhuri tunaona sio sababu ya kuahirisha kesi hii,” amedai.
Katuga amefafanua kuwa kifungu 192 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaeleza mahakama iwe ni ya wazi na kitu muhimu katika kesi hiyo mahakama itakubali kuwa na watu wanaosikiliza kesi hiyo ambao mahakama hiyo itakuwa inawamudu.
“Kwa ajili hiyo, usimamizi utatolewa kwa idadi ambayo sheria inasema na Mahakama itachukua kwa idadi ambayo inatakiwa na uwiano huo uliweka utaratibu wa idadi ya watu ambao wanatakiwa kuingia na kusikiliza kesi.”
“Lakini mahakama hii ina macho na imeona, kama kulikuwa na amri ya Polisi iliyotolewa hapa, kwa sababu mahakama pekee ndio yenye mamlaka ya kutoa amri,” amedai Katuga.
Katuga amedai hiyo ni mahakama ya wazi, kila mtu ana haki ya kuja mahakamani na kuondoka ndani ya mahakama ya wazi, hivyo haihitaji amri ya mahakama kuwarudisha watu walioondoka.
Amedai hakuna amri ambayo imetolewa mahakamani hapo zaidi ya mshtakiwa mwenyewe kueleza.
“Hii ni Mahakama ya wazi na Kila mtu yuko huru kuingia lakini wasiotaka hawalazimishwi, hivyo hoja ya mshtakiwa kuomba ahirisho kwa sababu hiyo si sababu ya msingi,” amesisitiza Wakili Katuga.
Lissu amesisitiza madai yake na Mahakama baada ya kusikiliza pande zote ndipo ikaahirisha kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa saa moja kwa ajili ya uamuzi.