Mwanza. Mikataba ya uonevu, ukosefu wa usalama kazini, kutojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kukosa bima za afya, likizo na mikopo, imetajwa kuwa changamoto kubwa zinazowakabili madereva wa bodaboda, bajaji na daladala nchini.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Septemba 16, 2025 na Ofisa Elimu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (Cotwu), Elisa Luvigo wakati akitoa mafunzo kwa sekta ya ajira isiyo rasmi kwa madereva bajaji, bodaboda na daladala jijini Mwanza.
Luvigo amesema utafiti uliofanywa jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 2024 na 2025 kwa madereva 159, wakiwemo wanawake 47, umebaini changamoto hizo ni za kitaifa na zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi.

“Tunawashauri wajiunge na vyama vya wafanyakazi ambavyo vitakuwa mwamvuli wao ili wapate urasimishwaji na stahiki kama bima ya afya na hifadhi ya jamii,” amesema Luvigo.
Ameongeza kuwa; “Hatupingi vikundi vyao bali tunaviwezesha kuwa na uwezo wa kukaa meza moja na Serikali kupitia Idara ya kazi.”
Mwenyekiti wa Cotwu Kanda ya Ziwa, Gigwa Muhule amesema lengo la mafunzo hayo ni kuandaa wasafirishaji wanaotambua haki na wajibu wao.
“Kwenye sekta zisizo rasmi watu wanachukuliwa kawaida, anaweza kupewa pikipiki leo na kesho akanyang’anywa. Tunataka wafahamu sheria, kanuni na taratibu ili wajilinde na kuendesha kazi zao kwa staha,” amesema Gigwa.
Kwa upande wake, Ofisa Miradi wa Shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES), Anna Mbise amesema sekta ya usafirishaji mdogo imekosa uratibu unaoeleweka hali inayosababisha madereva wengi kufanya kazi bila faida.
“Wengi wanakodisha vyombo kwa gharama kubwa, hawana maegesho rasmi na wanalipa tozo nyingi. Tunashirikiana na Cotwu kuelimisha na kukutana na wizara husika ili kuibua majadiliano yatakayowezesha mabadiliko ya sera na sheria,” amesema Mbise.
Katibu wa Madereva Bajaji Mkoa wa Mwanza (PCRO), Zakayo Mashamba amesema wamelipokea somo hilo kwa mikono miwili na wapo tayari kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

“Tunahitaji Serikali itusaidie tupate maegesho ya kudumu kwenye miji yetu hii na kupeleka huduma hizi hata vijijini kwa sababu hitaji la usafiri bado ni kubwa. Tunataka tuwe sehemu ya mpango wa Serikali wa urasimishaji ajira na tujulikane kisheria ili tuweze kulinda ajira zetu na kutetea haki zetu,” amesema Mashamba.
Ameongeza kuwa wanaamini mafunzo hayo yatasaidia kupunguza changamoto za mara kwa mara na kuongeza usalama wa huduma wanazotoa.
Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd amewataka wenzake kufuata kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kazi yao iwe endelevu.
“Semina ya leo imekuwa na elimu ya kutosha, tukiizingatia tutapata stahiki kama wafanyakazi wengine, lakini pia tutajengewa heshima na jamii na kuondoa mtazamo hasi unaotuona kama wahalifu barabarani,” amesema.
Ameahidi kushirikiana na vyama vya wafanyakazi na wadau wa usalama barabarani kutoa elimu kwa madereva wapya na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kazi wanazofanya.