MAFUNDO MCHUNDO WATAKIWA KUZINGATIA HIFADHI YA TABAKA LA OZONI

………………….

Serikali imewataka mafundi mchundo wa majokofu na viyoyozi kuendelea
kutumia njia salama za kuhudumia vifaa hivyo pasipo kuathiri mazingira na sanjari
na kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali zinazodhibitiwa.
 

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Deogratius Paul wakati akifungua mafunzo
kwa mafundi viyoyozi na majokofu wa Jiji la Dodoma kuhusu matakwa ya Itifaki ya
Montreal kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka
la Ozoni, leo Septemba 16, 2025.

Tanzania ni nchi mwanachama wa Itifaki ya Montreal ambao
unazitaka nchi hizo kutoa mafunzo kwa mafundi viyoyozi na majokofu kuhusu namna
bora ya kuhudumia vifaa hivyo pasipo kuachia angani kemikali zinazoweza
kusababisha uharibifu wa tabaka la ozoni au kuchangia ongezeko la joto duniani.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Paul
alisema kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni ni zile zinazotumika katika
majokofu na viyoyozi mbalimbali, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma,
utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na kilimo
cha maua, hifadhi ya nafaka katika maghala na kadhalika.

Dkt. Paul alieleza
kuwa kemikali hizo huingizwa nchini kupitia mipaka mbalimbali na zinaweza
kuharibu tabaka hilo au kuchangia
ongezeko la joto duniani hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi endapo
zikiachiwa angani.

“Tutambue kuwa
Tabaka la Ozoni kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua
isifike kwenye uso wa dunia, linapoharibiwa huruhusu mionzi ya jua kufika
kwenye uso wa dunia na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo
saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na
kujikunja kwa ngozi kuathirika kwa ukuaji wa mimea,” alisema.

Aidha, Dkt. Paul
ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Sehemu ya Hifadhi ya Bioanuai
aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya Ozoni kwa
wengine ili  kuongeza juhudi za kuhifadhi
Tabaka la Ozoni na hivyo kuokoa maisha duniani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Udhibiti
wa Uchafuzi wa Mazingira) Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Thomas
Chali alisema
madhumuni ya itifaki hiyo ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na
kumong’onyoka kwa tabaka la ozoni yanayotokana na uachiaji angani kemikali
zilizothibitishwa kuwa na kiwango kikubwa cha kuharibu tabaka hilo.

Aidha, Bw. Chali alifafanua kuwa kemikali zinazodhibitiwa
hutumika katika sekta mbalimbali kama vile majokofu na viyoyozi, kilimo,
shughuli za anga, viwanda vya madawa, viwanda vya magodoro na sekta ya uzimaji
moto.

Alibainisha kuwa nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 90 ya
matumizi ya kemikali hizi ni katika sekta ya majokofu na viyoyozi ambapo
hutumika kama vipozeo (refrigerants)
katika majokofu na viyoyozi.

Mafunzo hayo yamehusisha washiriki 40 wakiwemo mafundi
mchundo wa viyoyozi na majokofu kutoka kwenye kampuni binafsi,  Watoa mada kutoka:Ofisi ya Makamu wa
Rais,  Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA)-Chang’ombe na
Wakala wa Elimu ya
Mafunzo ya Uvuvi (FETA)–Bagamoyo.

Itakumbukwa kuwa
kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 2025 ni “Miaka
40 ya Mkataba wa Vienna: Mchango wa Sayansi kwenye Jitihada za kimataifa za
katika Hifadhi ya Tabaka la Ozoni
”.

Kauli mbiu hii
imechaguliwa kutokana na Mkataba wa Vienna unaohusu hifadhi ya tabaka la ozoni,
kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1985.