Mahakama yakataa madai ya Lissu

‎‎Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekataa madai na maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kuwa wafuasi wake waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake, wamefukuzwa katika ukumbi wa Mahakama inayosikilizwa kesi hiyo.

Lissu ametoa madai hayo leo Jumanne, Septemba 16,2025 kabla ya kuanza usikilizwaji wa sababu ya pili ya pingamizi lake la kupinga uhalali wa Mahakama hiyo kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Wakati kesi hiyo ilipoitwa baada ya majaji kuingia ukumbi wa wazi namba moja inakosikilizwa kesi hiyo, baadhi ya wafuasi wake viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema walinyanyuka kwa pamoja na kutoka nje ya ukumbi mahakama, huku wengine wachache wakibakia ndani ya ukumbi huo.

Kutokana na kitendo hicho Lissu aliieleza Mahakama kuwa wafuasi wake hao wamefukuzwa kutoka mahakamani kwa amri ya Ofisa wa Polisi na akaieleza Mahakama kuwa hayuko tayari kuendelea na kesi hiyo, huku akiomba ahirisho mpaka wafuasi wake hao watakapoitwa kuingia mahakamani.

Jamhuri kupitia kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amepinga madai hayo ya wafuasi wake kufukuzwa na maombi ya kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa sababu hiyo akisema kuwa hakuna amri yoyote iliyotolewa kuwafukiza.

Badala yake amedai kuwa wameondoka kwa ridhaa yao wenyewe na kama ingekuwepo amri hiyo mahakama ingeisikia kwani kitendo hicho limefanyika mbele yao na kuthibitisha kuwa hapakuwa na amri hiyo. Wakili Katuga amedai kuwa ndio maana wafuasi wake wengine walibakia mahakamani.

Mahakama katika uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za pande zote imeeleza kuwa madai hayo si ya kweli.

Akitoa uamuzi huo, kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Dunstan Ndunguru amesema kuwa baada ya kusikiliza madai na hoja za pande zote Mahakama imefuatilia kujua kama kuna hiyo amri kutoka kwa kiongozi wa polisi kuwaondoa watu mahakamani.

Hata hivyo Jaji Ndunguru amesema kuwa Mahakama haijapata amri yoyote kutoka Polisi ya kuwatoa watu ukumbini.

“Pia tukiwa mahakamani hapa tuliona namna watu walivyokuwa wananyanyuka na kama ingekuwepo amri hiyo, tungeisikia”, amesema Jaji Ndunguru.

Pia Mahakama hiyo imekubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa ingawa huo ni ukumbi wa wazi ambamo mtu yeyote anaruhusiwa kuingia kusikiliza mwenendo wa kesi, lakini ina ukomo haiwezi kuchukua watu zaidi.

Hivyo Mahakama imeelekeza kuwa ule utaratibu ambao umekuwa ukitumika awali auendelee na kama kuna tatizo liwasilishwe kwa Mahakama.

Jaji Ndunguru amesema kuwa wale waliokuwa mahakamani wangeendelea kuwepo na kama kuna tatizo lingepatiwa ufumbuzi kabla ya Mahakama kuanza.

Jaji Ndunguru amesisitiza kuwa kama kuna watu walitaka kutoka walipaswa watoke kabla ya Mahakama kuanza (majaji kuingia ukumbini) na kama wanakuwepo (wakati mahakama inaanza) waendelee kusalia hapo mpaka usikilizwaji wa kesi unapomalizika.

Lissuanakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Septemba 8, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la Majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde.

Hata hivyo Lissu aliibua pingamizi akiomba mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iitupilie mbali akitoa sababu mbili, ubatili wa hati ya mashtaka na mamlaka ya mahakama, ambayo mahakama hiyo jana Jumatatu, Septemba 15, 2025, imeikataa.

Baada ya Mahakama kulikataa sababu hiyo ndipo Lissu akaendelea na sababu hii ya pili ya pingamizi lake, yaani ubatili wa hati ya mashtaka, aliyoianza jana na kuendelea nayo leo Jumanne, Septemba 15, 2025.

Kabla ya kuanza usikilizwaji wa pingamizi lake hilo, ndipo akaibua madai hayo.

Kesi hiyo inaendelea sasa hivi ambapo Lissu anaendelea na hoja za pingamizi lake hilo.