……………
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa
Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu
Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Makamu
wa Rais amemsihi Balozi Mutatembwa kuzingatia kipaumbele cha nchi ambacho ni
diplomasia ya uchumi kwa kuhakikisha anavutia wawekezaji na wafanyabiashara
kutoka nchini Japan pamoja na kuimarisha ushirikiano wa ubia.
Amemsisitiza Balozi
Mutatembwa kuhakikisha makampuni ya Japan yanawekeza nchini Tanzania ili
kuongeza thamani ya bidhaa hapa nchini na kuuza katika soko la Japan na soko la
kimataifa.
Amesema ni vema kushawishi
wamiliki wa viwanda kuwekeza nchini Tanzania hususani viwanda vya magari, viwanda
vya dawa na vifaa tiba pamoja na viwanda vya bidhaa za kielektroniki.
Pia amesema kwa kuwa Japan
inafanya vizuri katika sekta ya lojistiki ni vema kuvutia ushirikiano kwa
kuzingatia kuwa Tanzania ni lango kwa mataifa mbalimbali.
Halikadhalika, Makamu wa
Rais amemtaka Balozi Mutatembwa kuvutia uwekezaji katika sekta muhimu za
kimkakati kama vile Utalii, Kilimo na Uvuvi pamoja na sekta ya Afya.
Amesema nchi ya Japan ni
wabobezi katika matibabu ya magonjwa yasiyoambukizia kama vile magonjwa moyo na
figo hivyo ni vema kuendelea kutafuta fursa za masomo ya ubobezi kwa Watanzania.
Pia ametaka kusimamia
utekelezaji wa vipengele vya Mpango wa Ushirikiano kati ya Japan na nchi za
Afrika pamoja na kusimamia hati za makubaliano na ushirikiano zilizopo baina ya
miji ya Tanzania na Japan.
Makamu wa Rais amemsihi
Balozi Mutatembwa kuwatambua na kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Japan
ikiwemo kuwaonesha fursa ya kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kuwekeza nchini
katika sekta ya makazi na biashara.
Vilevile amemtaka Balozi
Mutatembwa kuendeleza jitihada za matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Japan
na kutafuta fursa zitokanazo na Kiswahili kama vile walimu na wakalimani.
Makamu wa Rais amempongeza
Balozi Mutatembwa kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Japan. Amesema ni
muhimu kuhakikisha anakuwa na nyenzo muhimu zitakazomuongoza katika uwakilishi
nchini Japan ikiwemo Dira ya Taifa Maendeleo 2050, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
pamoja na takwimu za msingi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kwa upande wake Balozi
mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuiwakilisha
Taifa nchini Japan. Amesema atahakikisha analinda maslahi ya Tanzania na kuendelea
kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Japan.