KIPA wa Singida Black Stars, Metacha Mnata ameibuka kipa bora wa mashindano ya Kombe Kagame (Kagame Cup) yaliyofikia tamati jana Septemba 15, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mbali na Metacha, timu ya Al Hilal ya Sudan imetwaa tuzo ya ‘fair play’ katika mashindano hayo, tuzo waliyobidhiwa na mwakilishi kutoka Times FM, katika hafla ya utoaji tuzo (Gala Dinner) iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Septemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo iliyohudhuliwa na wachezaji, viongozi mbalimbali wa soka na wadau wa michezo, Metacha alikabidhiwa tuzo hiyo na
mkuu wa masoko na mawasiliano wa Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Andrew Jackson Oryada.
Akizungumzia mashindano hayo, Oryanda amesema msimu huu yamefanyika kwa kiwango bora, akiwashukuru wadau mbalimbali kwa kusapoti na kuyafanya kuwa bora zaidi.
“Radio mshirika wa Cecafa, Times FM ilirusha live (mubashara) kila hatua iliyofanyika uwanjani na hata nje ya uwanja, hii iliongeza hamasa ya mashindano,” amesema Oryanda.
Mwakilishi wa Times FM, Jacob Mbuya akikabidhi tuzo ya fair play kwa klabu ya Al Hilal, alisema msimu huu historia ya mashindano hayo imeandikwa kupitia radio hiyo, ambayo haikuishia tu kuwa radio bali daraja la maendeleo ya michezo kwa jamii.
“Kama radio mshirika wa Kagame Cup, hakuna tulichokiacha uwanjani au nje ya uwanja, mashabiki ambao hawakuweza kufika uwanjani walipata kile walichokitarajia kutoka kwenye mashindano haya laivu kupitia radio yao pendwa ya michezo nchini, Times FM.
“Hata baada ya Kagame Cup tutaendelea kuwapa taarifa bora za michezo kama radio pekee ya michezo nchini Tanzania kwa saa 24 kila siku, tukiwa daraja na injini ya maendeleo kwa jamii,” amesema.
Katika hafla hiyo, nyota wa APR ya Rwanda, Dao Rouaf Memei aliibuka MVP wa mashindano, huku kiungo Mzambia wa Singida Black Stars, Clatous Chama
akitwaa kiatu cha dhahabu kwa kuwa mfungaji bora wa mashindano.
Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi akitwaa tuzo ya kocha bora wa mashindano hayo akiwa ameiongoza Singida Black Stars kutwaa ubingwa kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal kwenye fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa KMC Complex jioni ya Septemba 15, 2025.
Mabingwa hao mbali na kombe, walikabidhiwa hundi ya Sh 25milioni kutoka kwa wadhamini, kampuni ya Betika.
APR ya Rwanda ilimaliza ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu.