Babati. Mgombea urais kupitia chama cha NLD Doyo Hassan Doyo amesema endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, atahakikisha madini ya Tanzanite yanawanufaisha wana Manyara kuliko hivi sasa.
Doyo ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 16, 2025, alipozungumza na wananchi wa maeneo ya Bonga, Hala, Nakwa, Sigino na Singu Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Amesema madini ya Tanzanite yanayopatikana katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani Manyara pekee duniani yanapaswa kuwanufaisha wanachi hao kwa kuwa yapo kwenye ardhi yao.
Mgomba huyo amesema wananchi wa Manyara hawajanufaika moja kwa moja na rasilimali hiyo licha ya kuwa madini hayo yanapatikana kwao pekee na kutoa mfano wa baadhi ya nchi za Kiarabu, ambazo wananchi hunufaika moja kwa moja na mafuta yanayopatikana nchini mwao kwa kuondolewa baadhi ya kodi.
“Iwapo angalau asilimia 40 ya mapato ya madini yangerudi moja kwa moja katika halmashauri za wilaya inayopatikana madina hayo, wananchi wangepata huduma bora za kijamii,” amesema Doyo na kuongeza;
“Nikichaguliwa kuwa Rais, nitahakikisha wananchi wa Manyara wananufaika na madini ya Tanzanite ambayo yanayopatikana kwenye mkoa huu,” amesema.
Mgombea urais huyo amelalamikia mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumika katika zao la mbaazi, akisema hauwanufaishi wakulima wadogo wa Manyara na Tanzania kwa ujumla.
Amesema wakulima hulima kwa gharama zao, hununua pembejeo kwa fedha zao na hulinda mashamba yao kwa gharama kubwa, ila wanapofika sokoni hulazimishwa kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa bei ya chini.
“Wakati mnapouza kilo kati ya Sh700 hadi Sh1,700 tu, wapo wanunuzi binafsi waliokuwa tayari kulipa hadi Sh3,500 kwa kilo, hii ni dhuluma kwa mkulima.
“Nikipewa ridhaa ya kuwa Rais, nitahakikisha mkulima anauza mazao yake kwa bei ya soko huru na si kwa kulazimishwa na mfumo wa stakabadhi ghalani, unaonufaisha watu wachache,” amesema Doyo.
Amesema bei ya mbaazi imeshuka kutoka Sh3,000 kwa kilo hadi Sh700 hali iliyosababisha gunia la mbaazi kushuka kutoka wastani wa Sh300,000 hadi Sh70,000 pekee.
Amesema hali hiyo ni mzigo mkubwa kwa wakulima wa Manyara na mikoa mingine inayozalisha zao hilo nchini.
Amewataka wananchi wa Manyara kufanya uamuzi sahihi ifikapo Oktoba 29, mwaka huu kwa kumpa kura zoe za ndiyo ili awe rais sambamba na mgombea ubunge wa Babati Mjini kupitia NLD, Paschal Ngomuo na mgombea udiwani Kata ya Babati, Andrea Kiula.
Amesisitiza kuwa Manyara itakuwa kituo cha utalii baada ya Arusha na vijana wa Babati watanufaika na fursa za kiuchumi kupitia utalii.
Mgombea ubunge wa Babati Mjini kupitia NLD, Paschal Bruno Ngomuo, amesema wananchi wamepewa nafasi ya kuchagua kiongozi sahihi atakayepigania maslahi yao hivyo wachukue hatua.
Ameahidi kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha geti la Mamire linatambulika kama lango la utalii, tofauti na ilivyo sasa ambapo wageni wengi hutumia Minjingu na kibao cha tembo karibu na Magugu.
“Wananchi wa Babati, kupanga ni kuchagua, mkinichagua mimi nitakuwa sauti yenu, nitalinda maslahi yenu na kuhakikisha mnafaidika na bei nzuri za mazao yenu, mkiendelea kuchagua viongozi wa sasa, mtabaki na bei zisizo na faida kwenu,” amesema Ngomuo.
Kesho Jumatano Septemba 17, 2025, Doyo ataendelea na kampeni zake Arusha mjini ambako atafanya mikutano kadhaa.