Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kufanya mageuzi katika sekta ya uvuvi ikiwemo kuboresha miundombinu ya bandari na masoko ya samaki ili kuongeza kipato cha wavuvi.
Othman amefafanua kuwa maboresho hayo yatawezesha wavuvi kupata sehemu nzuri za kuhifadhia mazao yao ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Ameeleza hayo leo Jumanne, Septemba 16, 2025, katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni akianzia Kijiji cha Makangale, wilayani Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Katika mkutano huo, Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, alipokea kero mbalimbali kutoka kwa wavuvi wa Bandari ya Mnarani na kuzipatia ufumbuzi.

Akihutubia wananchi hao katika mkutano wa hadhara, Othman amesema amedhamiria pia kutoa mikopo nafuu na zana za kisasa, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato cha wavuvi.
“Serikali ya ACT Wazalendo itawekeza katika teknolojia ya usindikaji na hifadhi ya samaki, ili kuongeza thamani ya bidhaa na kufungua fursa za ajira.
“Tutalinda mazingira ya bahari na kudhibiti uvuvi haramu, sambamba na kutoa elimu kwa jamii za wavuvi juu ya utunzaji wa rasilimali,” amesema Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Katika mkutano huo, wavuvi wa Bandari ya Mnarani wameelezea kero zao mbalimbali, ikiwemo gharama za vifaa vya uvuvi, uhaba wa masoko ya uhakika na ukosefu wa hifadhi bora ya samaki.
Ali Said Ramadhan, amedai kumekuwa na unyanyasaji unaofanyika kwa kisingizio cha uhifadhi wa maeneo ya kuvulia, akisema mara kwa mara wavuvi wananyang’anywa nyavu zao.
“Tumechoka kunyanyaswa, vifaa vyote tunavyovitumia tunavichukua kwa mikopo, sasa nyavu zikiharibiwa tutalipia nini?” amehoji Ramadhan.
Akijibu hoja hiyo, Othman amesisitiza kuwa sekta ya uvuvi ndiyo uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar, na Serikali atakayoiunda akishika dola itahakikisha haki na maslahi ya wavuvi yanalindwa.
“Serikali ya ACT Wazalendo itaweka sekta ya uvuvi katika kipaumbele cha kwanza, kwa sababu maendeleo ya Zanzibar hayawezi kujengwa bila kumuinua mvuvi,” amesisitiza Othman.

Aahidi kukuza, kulinda utalii
Katika hatua nyingine, Othman amesema Serikali atakayoiunda itahakikisha utalii unaolinda mazingira na maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufanywa kwa kuharibu jamii.
“Tutakuwa na utalii wa kimazingira, lazima tuwe na viwango vya hoteli. Tunataka kila hoteli iende sambamba na uhalisia wa eneo na fursa zake.
“Hatuwezi kujenga hoteli katikati ya kijiji, hii itaharibu maisha ya wananchi na utamaduni wetu. Tutahakikisha maeneo ya maendeleo ya utalii yanapangwa kwa busara ili kulinda fukwe, misitu na urithi wa kijamii,” amesema Othman.