Polisi Ruvuma yapokea magari 24 kuimarisha ulinzi na usalama

Songea. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed amekabidhi magari 24 kwa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma ambapo amewaagiza kufanya kazi kwa kufuata weledi na utii.

Amewaasa pia  wawahudumie wananchi kwa hekima na busara.

Akikabidhi magari hayo leo Septemba 16, 2025 Ahmed amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa magari 24 mapya awamu ya kwanza magari tisa na awamu ya pili magari 15 ya kisasa, ambapo lengo ni kulipatia Jeshi la Polisi vifaa ili wafanye kazi kwa weledi.


“Namshukuru IGP kwa uboreshaji wa Jeshi la Polisi pamoja na vifaa walivyotoa vitasaidia kwenye uchaguzi kufanya kazi kwa weledi, umakini na utulivu,” amesema.

Aidha, amempongeza Kamanda wa Polisi kwa kazi kubwa wanayofanya ya kulinda amani ndani ya mkoa na Taifa kwa ujumla ambapo amewataka Polisi wavitumie kwa usahihi na umakini mkubwa, pia  wayafanyie matengenezo kila inapohitajika na washirikiane kulinda Taifa.


“Ili tuwe na Jeshi imara nitoe rai kwa maofisa wa Polisi na askari kujiendeleza kielimu ili kwenda na wakati,” amesema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa Ruvuma, Marco Chilya amesema wamekabidhiwa magari yaliyotolewa na Rais kwa ajili ya vitengo mbalimbali vikiwamo vya Kamanda, Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia, Mkuu wa Upelelezi na wakuu wa Polisi Wilaya.