Sekondari ya Temeke yapigwa tafu vifaa vya maabara

Dar es Salaam. Katika kutekeleza mkakati wa kuinua ubora wa elimu ya sayansi nchini Tanzania, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa msaada wa Sh10 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika Shule ya Sekondari Temeke.

Fedha hizo zimekabidhiwa shuleni hapo, kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara na kemikali zinazotumika kwenye majaribio ya kisayansi.

Akizungumza leo Septemba 16, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dk Bill Kiwia amesema taasisi yake imeona umuhimu wa kushiriki moja kwa moja katika kuboresha elimu ya ngazi ya sekondari, kwa kuwa ndiyo msingi wa wanafunzi wengi wanaokuja kuomba mikopo ya elimu ya juu.


“Taasisi yetu mara nyingi imekuwa ikihusishwa na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pekee, lakini tumeona kuwa hatuwezi kufanikisha jukumu letu bila kushirikiana katika hatua za awali za safari ya elimu. Wanafunzi wanapokuwa na mazingira bora ya kujifunza masomo ya sayansi, itawasaidia kupata ufaulu mzuri na hatimaye kuwa wabunifu na wanasayansi bora,” amesema Dk Kiwia.

Ameongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo kushirikiana na jamii, kwa kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi na yenye tija.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Ingia Mtenga amesema msaada huo umekuja  wakati muafaka kwani shule yake kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia masomo ya sayansi.


“Kwa muda mrefu wanafunzi wetu wamekuwa wakijifunza kwa nadharia zaidi badala ya vitendo kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kutosha maabara. Hali hii mara nyingine imekuwa ikipunguza ari ya wanafunzi katika masomo ya sayansi. Tunashukuru sana kwa msaada huu ambao tunaamini utaongeza ufaulu na hamasa ya wanafunzi wetu,” amesema.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwananchi wameeleza kuwa msaada huo utawapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kuelewa vyema masomo ya sayansi.

“Hapo awali tulikuwa tunajifunza zaidi kwa kusikia na kusoma vitabuni, lakini sasa tutakuwa na vifaa vya kufanya majaribio na kujionea matokeo. Hii itatupa uelewa wa kina zaidi,” amesema Asha Ally, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo.

Naye Baraka Joseph, mwanafunzi wa kidato cha sita, amesema msaada huo utawasaidia kujiandaa vizuri kwa mitihani ya Taifa.


“Mitihani ya sayansi ina sehemu kubwa ya vitendo, kwa hiyo tutapata maandalizi bora na kuondoa hofu tuliyokuwa nayo awali,” amesema.

Msaada huo umetajwa kuwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali na wadau wengine kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na maabara iliyo kamili, sambamba na Sera ya Elimu inayotaka kusisitiza ujuzi wa vitendo katika kujifunza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari nchini zinakuwa na maabara zenye vifaa vya kisasa ifikapo mwaka 2030, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi na teknolojia.

Msaada huu unaonyesha mshikamano wa taasisi za Serikali katika kuunga mkono dira ya Taifa ya kukuza elimu bora, ubunifu na sayansi kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda na uchumi wa maarifa.