Sh51 bilioni zaboresha miradi ya kimkakati Jiji la Mbeya

Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh51 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwepo masoko, kituo cha kisasa cha mabasi ya mikoani, machinjio na barabara kwa kiwango cha lami katika Jiji la Mbeya.

Miradi hiyo inatekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (Tactics), chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji (Tarura) kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Dunia.

Mratibu wa Mradi Tactics, Yunus Nsegobya ameliambia Mwananchi leo Jumanne Septemba 16, 2025 wakati akizungumzia utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa jamii.

Amesema kwa upande Jiji la Mbeya wametekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 12.3, mitaro ya maji ya mvua kilometa 6.41 na ufungaji wa taa za barabarani.


Miradi mingine ni ujenzi wa jengo la ofisi ya kusimamia mradi litakalogharimu Sh21 bilioni ambao umefikia asilimia 70 na kituo kikubwa cha mabasi ya mikoani eneo la Old Airport, chenye thamani ya Sh30 bilioni.

“Miradi hiyo ikikamilika itawezesha halmashauri ya Jiji la Mbeya kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh24 bilioni mpaka kati ya Sh35 bilioni na 40 bilioni,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema hatua ya Serikali kuboresha miundombinu ya barabara imepandisha uwezo wa wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kwa kusafiri na kusafirisha bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Wakati huohuo, Nsegobya amewataka wananchi kutumia vizuri miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu kwa masilahi yao na Taifa kwa ujumla.


Naye Meneja wa Tarura Wilaya ya Mbeya, Boniface Kasambo ametaja miradi mingine ni ujenzi wa Barabara ya Uyole – Itezi yenye urefu wa kilometa 1.8, Kabwe – Block T kilometa 1.2 na Barabara ya Iziwa yenye urefu wa kilometa 2.

Nyingine ni Barabara ya Kalobe yenye urefu wa kilometa 3.8 na mfereji wa kupitisha maji ya mvua wenye urefu wa kilometa 6.41, hatua ambayo amesema italeta tija kwa wakulima kufikisha mazao yao kwenye masoko kwa urahisi.

“Kimsingi uwekezaji huo wa Serikali umeleta tija kubwa katika maeneo mbalimbali na kuondoa adha ambayo ilikuwa changamoto kwa wananchi,” amesema.

Mkazi wa machinjioni eneo la Veta jijini hapa, Victoria Mlay amesema hatua ya Serikali kuboresha miundombinu ya barabara na masoko umeleta tija na kufungua fursa za kiuchumi na kibiashara na urahisi wa usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Miaka ya nyuma barabara ilikuwa changamoto, ukitaka kufika machinjio ya veta watu wanatafuta njia za mkato, lakini sasa ni lami tupu, kimsingi naipongeza Serikali kwa uwekezaji huu,” amesema.

Mfanyabiashara wa Soko la Matola, Zena Nassoro amesema ujenzi wa soko jipya la kisasa la Matola litakuwa kivutio kwa watu kutoka maeneo mbalimbali na kuchochea kasi ya shughuli za kiuchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja.

Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari Uyole, Ezekiel Gwenino amesema katika msimu wa mvua barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na mashimo, matope na maji kujaa na kusababisha vyombo vya moto kutofikika kirahisi, jambo linalokwenda kumalizika.

Aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya na mgombea udiwani Kata ya Isanga, Dourmohamed Issa amesema utekelezaji wa miradi hiyo unabadili taswira ya Jiji la Mbeya hususani ujenzi wa masoko, kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na barabara.