Dodoma. Mtalaa ulioboreshwa ulioandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) unaendelea kutekelezwa.
Pamoja na mambo mengine, lengo la mtalaa huu ni kuhama kutoka kumkaririsha mwanafunzi maarifa kwa minajili ya kufaulu mitihani, kwenda kwenye hatua ya kumwezesha mwanafunzi kupata mahiri zinazoweza kumsaidia kuendesha maisha yake hata baada ya masomo.
Hatua hii kwa hakika, ni muhimu kwa sababu jamii ya sasa inahitaji wahitimu wabunifu, wenye uwezo wa kutatua matatizo, kushirikiana, na kujiamini katika kufanya uamuzi.
Ikumbukwe kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko kuwa wanafunzi wengi wanamaliza shule, lakini hawana ujuzi unaowasaidia kuendesha maisha yao.
Hata hivyo, utekelezaji wa mtalaa huu unategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa mwalimu kutengeneza shughuli za ujifunzaji zinazomshirikisha kikamilifu mwanafunzi.
Uzoefu wa walimu unaonesha kuwa kutafsiri shughuli za ujifunzaji zinazopendekezwa kwenye mtalaa katika mazingira ya darasani, imekuwa kazi kubwa kama anavyoeleza mwalimu Grace Charles wa Chuo cha Ualimu Marangu:
“Mtalaa huu una malengo mazuri lakini nina shaka na namna tunavyoutekeleza. Unakuta ile shughuli inayopendekezwa kwenye mtalaa unaifundisha kwa kipindi kifupi na mada ikaisha. Inakuwa vigumu kuelewa badiliko hasa liko wapi kwenye huu mtalaa?”
Anachokisema mwalimu Grace kinaonesha uwepo wa pengo kati ya wakuza mitalaa na watekelezaji.
Kwa mfano, wakati wakuza mitalaa wanachora picha ya aina ya mwanafunzi wanayemtarajia, kinachofanywa na mwalimu darasani kinashindwa kukamilisha picha hiyo iliyokusudiwa.
“Ukiangalia mabadiliko haya yanayozungumzwa kwenye mitalaa, unaona ni misamiati mipya tu tunapewa lakini mambo ni yaleyale. Mada zimebadilika zimekuwa umahiri. Malengo ya ujifunzaji yamegeuzwa na kuwa mahiri na shughuli za ujifunzaji. Hakuna kilichobadilika,” anasema mwalimu Mzava wa Shule ya Sekondari Nyehunge, Buchosa, wilayani Sengerema.
Naye Dorcas Kimambo, mwalimu wa shule ya sekondari Mawenzi mjini Moshi naye anaeleza mkanganyiko huu vizuri:
“Mtalaa mpya umeondoa mada ndogo na malengo ya somo. Badala yake kuna mahiri na shughuli za ujifunzaji. Darasani tunachofanya ni kuhamishia shughuli za ujifunzaji zinazoonekana kwenye muhtasari wa somo na kuzileta kwenye andalio la somo. Matokeo yake unaishia kutoa mhadhara badala ya kumshirikisha mwanafunzi kwa sababu unakuta haitekelezeki.”
Inavyoonekana, changamoto moja wapo, ni ukweli kuwa walimu wamezoea kufundisha maudhui kwa mbinu zisizo shirikishi.
Kwa msingi huo, pamoja na shauku ya kutekeleza mtalaa huu, walimu wengi hujikuta wakiishia kutumia mbinu zile zile na kufikiri kilichobadilika kwenye mtalaa mpya ni muundo wa uandishi wa andalio la somo.
Makala haya yanakusudia kuonesha namna gani utekelezaji wa mtalaa huu unategemea, kwa kiasi kikubwa, uwezo wa mwalimu kubuni shughuli bora ya ujifunzaji na kutoa mwongozo wa jumla wa namna ya kufanya hivyo.
Shughuli za ujifunzaji, kitaalamu, ni zile kazi anazopewa mwanafunzi zinazolenga kuwezesha mchakato wa kujenga mahiri mpya. Shughuli hizi zimegawanyika katika makundi makubwa matatu.
Kwanza, ni shughuli za kupata taarifa (absorb activities).
Hizi ni zile shughuli zinazomsaidia mwanafunzi kupata taarifa mpya, kwa kujenga msingi wa maarifa na kumwandaa kwa hatua nyingine ya ujifunzaji.
Taarifa hizi mwanafunzi huzipata kupitia kusoma, kuangalia au kusikiliza. Umuhimu wa shughuli hizi unatokana na ukweli kuwa bila mwanafunzi kupata taarifa za awali, inakuwa vigumu kushiriki kikamilifu katika uundaji wa maarifa mapya.
Shughuli za kuunda maarifa (Do activities), kwa upande mwingine, hufanya zoezi la kumhamisha mwanafunzi kutoka kwenye ngazi ya taarifa hadi kujenga maarifa mapya.
Hizi ni shughuli zinazomhusisha mwanafunzi moja kwa moja katika kutenda na hivyo mwanafunzi anakuwa si msikilizaji pekee bali ni mshiriki mkuu anayejenga uelewa wake kupitia vitendo kama majaribio, mijadala au kazi za kikundi.
Shughuli hizi humpa mwanafunzi nafasi ya kujaribu, kukosea, na kujifunza tena, hali inayomjengea ujasiri na ubunifu.
Kisha kuna shughuli husianishi, ama ‘connect activities’ zinazomsaidia mwanafunzi kuunganisha alichojifunza na uhalisia wa maisha ya kila siku. Shughuli hizi huunganisha somo la darasani na uhalisia wa jamii.
Kupitia shughuli hizi, mwanafunzi huona maana ya kile anachojifunza kwa kuwa kinamgusa moja kwa moja katika maisha yake ya kila siku.
Kila shughuli ya ujifunzaji, iwe ya kupata taarifa, kuunda maarifa au kuhusianisha, huongozwa na sifa kuu tano. Sifa hizi ndizo zinazotofautisha shughuli ya ujifunzaji na swali la kawaida la kitabu.
Ikumbukwe walimu wengi huchanganya kati ya swali la kupima uelewa na shughuli ya ujifunzaji. Bila uelewa wa sifa hizi, mwalimu anaweza kutoa kazi ya kawaida ya darasani isiyochangia kukuza mahiri. Tutazame sifa hizo moja baada ya nyingine.
Shughuli bora lazima imwonyeshe mwanafunzi kazi mahsusi ya kufanya. Shughuli isiyoeleza kazi humwacha mwanafunzi bila mwelekeo, humfanya mwalimu kushindwa kupima ufanisi. Kazi yenye uwazi humfanya mwanafunzi ajue kinachotarajiwa na kumpa mwalimu kipimo cha uhakika.
Kwa mfano, katika somo la sayansi, badala ya mwalimu kusema: “Jadili seli za mimea na wanyama,” anaweza kumpa kazi mahsusi inayoainisha atafanya nini kupata taarifa au kuchambua taarifa hizo kujenga maarifa na ujuzi mpya.
Shughuli nzuri inasomeka kama ifuatavyo: “Soma matini uliyopewa ukurasa wa 45 kisha chora mchoro unaoonyesha tofauti tatu kati ya seli za mimea na wanyama.” Shughuli kama hii humwonyesha mwanafunzi atafanya nini kwa umahususi.
Shughuli isipoeleza kazi mahsusi inayotakiwa kufanyika, husababisha mwanafunzi kuishia kutoa majibu ya jumla yasiyotokana na uelewa mpya alioupata kwa kujifunza.
Matokeo yake mwanafunzi anaweza kushindwa kujifunza na hata akijifunza itakuwa vigumu kufanya tathmini ya kile alichojifunza.
Shughuli bora huonesha wazi nyenzo zitakazotumika. Nyenzo, zamani zikiitwa zana za kufundishia, ndizo hufanya ujifunzaji uwe hai na wa kweli.
Bila nyenzo, shughuli hubaki katika nadharia na humfanya mwanafunzi ajisikie anatarajiwa kujua kile ambacho kimsingi anapaswa kujifunza.
Kwa mfano, katika somo la historia, mwalimu anapopanga wanafunzi wachambue Mkutano wa Berlin, anapaswa kuwapa ramani, makala au picha za kihistoria. Hii huwasaidia wanafunzi kuchanganua tukio kwa kutumia ushahidi wa kitu halisi.
Kukosa nyenzo hufanya wanafunzi kushindwa kushiriki kikamilifu. Badala ya kuchambua kwa uhalisia, wanaishia kutoa maoni ya jumla yasiyo na mashiko.
Shughuli bora hulenga kukuza mahiri maalum badala ya kuishia kwenye maarifa pekee.
Ikumbukwe kuwa mtalaa mpya unalenga kukuza mahiri kama ubunifu, ushirikiano, ushirikeli, fikra tunduizi, utatuzi wa matatizo, mawasiliano au uzalendo.
Bila kufafanua mahiri zinazokuzwa, shughuli hubaki katika kiwango cha maarifa ya nadharia pekee na haitomsaidia mwanafunzi kujenga mahiri zinazokusudiwa kwenye mtalaa.
Kwa mfano, katika somo la hisabati, wanafunzi wakipewa kazi ya makundi kupima eneo la shamba dogo nje ya darasa, hawajifunzi tu vipimo bali pia ushirikiano na mawasiliano wanapogawana majukumu.
Shughuli isipojikita kwenye mahiri husika, mwanafunzi anaweza kufaulu mtihani lakini akashindwa kutumia maarifa hayo katika maisha ya kila siku.
Shughuli lazima ionyeshe wazi mbinu itakayotumika kuitekeleza. Je, shughuli hiyo itafanywa na mwanafunzi mmoja mmoja, wawili wawili au vikundi? Je, shughuli hiyo itatekelezwa ndani au nje ya darasa?
Kuainisha namna shughuli itakavyotekelezwa huongeza uwezekano wa shughuli hiyo kufanyika kama ilivyopangwa na hivyo kufanikisha lengo la ujifunzaji. Bila mbinu, mwalimu hushindwa kuelekeza wanafunzi ipasavyo.
Kwa mfano, katika somo la sayansi, mwalimu anaweza kupanga jaribio la kikundi ambapo kila mwanafunzi ana jukumu linaloeleweka.
Mmoja anapima, mwingine anandika matokeo, na mwingine anawasilisha. Hapa kila mwanafunzi hushiriki kwa nafasi yake.
Shughuli isipoeleza mbinu, wengine hubaki wasikilizaji bila kushiriki. Matokeo yake ni kupoteza fursa ya kukuza stadi za kijamii na kushirikiana.
Shughuli bora lazima iwe na kipimo cha wazi cha matokeo yanayokusudiwa katika shughuli husika. Upimaji hufafanua matarajio ya mwisho shughuli ikikamilika na huonesha kiwango cha ufanisi kinachotarajiwa.
Bila kigezo cha upimaji, mwalimu hawezi kuthibitisha ikiwa mwanafunzi amefanikisha malengo ya shughuli hiyo.
Mfano, katika somo la Kiswahili, mwanafunzi akipewa kazi ya kuandika barua ya maombi ya kazi, kipimo cha upimaji kinaweza kuwa: “barua iliyoandikwa ina anuani sahihi, imeandikwa kwa lugha sanifu na ina mpangilio wa barua rasmi.”
Kukosa upimaji huacha shughuli ikielea bila mwelekeo. Unapowaambia wanafunzi wachunguze, wasikilize, utapata tabu kupata ushahidi unaoonesha kama kweli wamechunguza au wamesikiliza.
Katika mazingira kama haya, mwanafunzi hatoweza kuelewa kipimo cha ujifunzaji na mwalimu, kadhalika, hushindwa kutoa mrejesho wa maana.
Ubora wa shughuli ya ujifunzaji, kwa hakika, ndio moyo wa ufundishaji unaojikita katika kukuza mahiri.
Mafunzo ya walimu katika kutekeleza mtalaa huu ni muhimu yasiishie kwenye uelewa wa muundo wa andalio la somo bali kumwezesha kuandaa shughuli za ujifunzaji zinazokidhi vigezo vilivyoainishwa.
Mwalimu akiweza kufanya hivi, anakuwa ametafsiri mtalaa mpya kwa vitendo katika mazingira ya darasani.
Mwandishi ni mdau wa elimu, mshauri elekezi na mhadhiri wa saikolojia ya ujifunzaji, Chuo Kikuu cha Dodoma.