Simba, Yanga zapishana dakika 12 kwa Mkapa

TIMU za Simba na Yanga tayari zipo ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaoanza saa 11:00 jioni.

Yanga ndio imekuwa ya kwanza kufika hapa Benjamin Mkapa ikiwasili saa 9:22 alasiri, lakini ikashtua kidogo.

Kilichofanyika, Yanga ikaibukia kusikojulikana ikitokea kwenye moja ya njia ya vumbi, kisha walinzi wake wakafungua kwa nguvu geti moja  dogo pembeni kidogo ya geti kubwa kisha basi lao kubwa likatumia hapo kupita kwa haraka.

Wakati Yanga ikipambana kuvunja uzio huo wa mageti ya chuma yale ya kuhamishika, askari waliokuwepo kulinda usalama hawakushtukia mapema, lakini baada ya kugundua wakaanza kukimbia kwenda kuwazuia.

Hata hivyo, askari hao hawakuwahi, walipofika wakalikuta basi la Yanga linamalizia kuingia na kuzusha majibizano makali.

Dakika 12 baadaye kwa maana ya saa 9:34 alasiri, Simba ikawasili uwanjani na kama ilivyokuwa Yanga, nayo ikatumia geti moja dogo karibu na mwisho wa uwanja, kisha kuelekea eneo lililo karibu na chumba wanachofikia kwenda kujiandaa na mchezo.

Wakati Simba nayo ikitumia geti hilo dogo wakiongozwa na makomandoo wao, askari pia walijikuta wameshindwa kuwadhibiti kwa haraka.

Katika hali ya kushangaza, wakati askari hao wakikutana na wakati huo mgumu kuzidhibiti timu zote zikitumia mageti sio rasmi, misafara ya vikosi vyote iliongozwa na pikipiki maalum za jeshi hilo zinazotumika kuongozea misafara.

Baada ya kufika, Yanga pia ikawa ya kwanza kuingia sehemu ya kuchezea kukagua ambapo ilikuwa saa 9:39 alasiri, kisha Simba ikafuatia saa 9:45 alasiri.