Watupwa jela wakituhumiwa kupanga kumuua rais kichawi

Lusaka. Mahakama kuu nchini Zambia imewahukumu wanaume wawili kifungo cha miaka miwili na miezi sita jela baada ya kuwakuta na tuhuma za kujaribu kumuua Rais wa taifa hilo Hakainde Hichilema kwa kutumia uchawi.

Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao Leonard Phiri na Jasten Mabulesse Candunde walitiwa hatiani chini ya Sheria ya Uchawi baada ya kukamatwa Desemba wakiwa na hirizi na kinyonga aliye hai.

Taarifa kutoka nchini humo zinasema watuhumiwa hao ambao pia ni waganga wa kienyeji  walikamatwa mwaka jana wakiwa katika mipango ya mwisho ya kukamilisha jukumu hilo ambalo walidai kuagizwa na kiongozi wa serikali.

Hakimu wa Mahakama hiyo, Fine Mayambu amesema watuhumiwa hao hakuwa adui kwa mkuu wa nchi pekee lakini pia walikuwa maadui kwa Wazambia wote, kwani walilenga kutokomeza uhai wa kiongozi wa mkuu wa taifa.

“Watuhumiwa hao walikubali umiliki wa hirizi hizo, Phiri alionyesha zaidi kwamba mkia wa kinyonga, ambao umechomwa na kutumiwa katika tambiko, ambao ulitegemewa ungesababisha kutokea kwa kifo cha rais wetu,”amesema Mayamba.

Mayamba ameongeza kuwa wametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho na onyo kali kwa wananchi wote wa Zambia kuhakikisha kuwa kosa hilo halijirudii.

Hata hivyo, wakili wa watuhumiwa hao, Agrippa Malando amesema wateja wake waliomba kuhurumiwa kwa kuwa walikuwa wakosaji kwa mara ya kwanza.

Wakili huyo pia alidai kuwa ni kweli wateja wake walifanya kitendo hicho lakini walifanya kama sehemu ya kazi yao ya kila siku ambayo walitumwa na miongoni mwa wabunge wa taifa hilo ambaye hajatiwa hatiani.

Hakimu Mayambu pia alitoa wito kwa Wazambia kuacha tabia ya kuamini uchawi na ushirikina katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia, huku akiongeza kuwa sheria ya taifa hilo iliundwa ili kulinda jamii dhidi ya hofu na madhara yanayosababishwa na wale wanaodai kuwa na uwezo wa kufanya vitendo vya uchawi.