YANGA imewaweka nje wachezaji wapya wote, ikianza na kikosi chenye wenyeji huku Simba ikija na wapya watatu.
Yanga inacheza dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii unaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kwenye kikosi cha Yanga kilichoanza, hakuna ambaye amesajiliwa dirisha kubwa lililofungwa Septemba 7 mwaka huu.
Kwenye ukuta wa Yanga, wameanza na kipa Djigui Diara, mabeki Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.
Viungo Aziz Andabwile ambaye anaanza kwa mara ya kwanza dhidi ya Simba licha ya kuwepo ndani ya timu hiyo tangu msimu uliopita, akicheza sambamba na Mudathir Yahya, Duke Abuya, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua.
Kule mbele Yanga imemuanzisha mshambuliaji Prince Dube huku mastaa wapya saba wakiwa benchi ambao ni Lassine Kouma, Abdulnasir Mohammed ‘Casemiro’, Moussa Bala Conte, Mohamed Doumbia, Celestin Ecua na Abubakar Nizar ‘Ninju’.
Wengine walioko benchi ni Clement Mzize, Bakari Mwamnyeto, huku Andy Boyeli, Frank Assinki na Edmund John ambao wamesalijiwa hivi karibuni wakiwa jukwaani.
Simba wao wameanza na wachezaji watatu wapya kwenye kikosi chao huku nane wakiwa wale waliokuwepo msimu uliopita.
Golini kuna Moussa Camara, mabeki ni Shomari Kapombe, Abdulrazack Hamza, wakati Rushine de Reuck na Naby Camara wanaokamilisha safu hiyo wakiwa wapya.
Kwenye kiungo kuna mtu mpya mmoja Alassane Kante, akicheza sambamba na wenyeji Yusuf Kagoma, Elie Mpanzu, Kibu Denis, Jean Charles Ahoua huku mshambuliaji akiwa Steven Mukwala.
Kwenye benchi la Simba sura mpya ni Yakoub Suleiman, Antony Mligo, Seleman Mwalimu, Morrice Abraham, Neo Maema na Wilson Nangu, wenyeji ni Ladacka Chasambi na Mzamiru Yassin.