Dar es Salaam. Wakati waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania na duniani wakiomboleza kifo cha Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, mwalimu na rafiki yake wameeleza namna atakavyokumbukwa.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Mwijage, katika tanzia kwa maaskofu, mapadri, watawa na waamini leo Septemba 17, 2025 amesema Askofu Mkuu Rugambwa alifariki dunia jana Septemba 16, jioni akipatiwa matibabu Roma, nchini Italia.
“Poleni sana na tuzidi kuiombea roho yake ipate pumziko la milele. Mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa,” amesema Askofu Mwijage.
Juni 10, 2025, akiwa mgonjwa Askofu Mkuu Rugambwa alishiriki mkutano wakati Papa Leo XIV, alipokutana na mabalozi wote wa Vatican wanaomwakilisha maeneo yote duniani. Alikuwa akitumia kitimwendo.
Kwa nyakati tofauti, Askofu Msaidizi mstaafu, Methodius Kilaini na Mosinyo Gosbert Byamungu, wakizungumza na Mwananchi wameeleza namna wanavyomkumbuka Askofu Mkuu, Rugambwa.
Wanaeleza akiwa kijana wa miaka 24, alikwenda Roma kwa masomo ya shahada ya falsafa kwa miaka mitatu. Aliporejea aliendelea na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadri mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.
Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, tangu akiwa shuleni, Rugambwa alikuwa mwenye akili: “Nilimfundisha alipokuwa kidato cha pili Seminari ya Rubya, Bukoba. Pia nikamfundisha historia ya kanisa alipokuwa Frateri. Darasani alikuwa wa kwanza au wa pili.”
“Nilimuona tena alipokuwa Roma akijifunza. Alipomaliza falsafa badala ya kwenda shule za kwetu, akatumwa Roma ambako ndiko alitokea na kuja kupata upadirisho mwaka 1986,” amesema.
Askofu Kilaini amesema Roma walikuwa wakitafuta vijana wenye akili, maadili na wenye utaua ili kufanya kazi za Baba Mtakatifu na kuwa Rugambwa alikuwa miongoni mwao.
Amesema kote ambako alipita alifanya kazi nzuri, hata Roma alikokwenda kusoma walipomuona na namna alivyokuwa na akili wakamuomba, wakampeleka shule ya diplomasia alikoanza kazi hiyo.
“Amezunguka nchi nyingi kama katibu wa balozi wa Baba Mtakatifu, baadaye akawa balozi wa Baba Mtakatifu nchini Angola na maeneo mengine mengi,” amesema.
Amesema alianza kuugua akiwa New Zealand alipopata nafuu alipelekwa Roma.
“Ni juzi juzi tu (Juni 10, 2025) alipokewa na Baba Mtakatifu japo alikuwa kwenye wheelchair (kitimwendo), lakini alikuwa anaongea, baadaye alipata kiharusi hadi kupoteza maisha,” amesema Askofu Kilaini akimtaja Mosinyo Byamungu kuwa ni miongoni mwa vijana waliokuwa na akili darasani alipowafundisha mwaka 1973 na kupelekwa Roma pamoja na Rugambwa.
Kwa upande wake, Mosinyo Byamungu aliyesoma na Rugambwa na kuwa pamoja katika majiundo ya kikasisi, anamwelezea mwenzake kuwa, alikuwa akifahamu sana hesabu.
“Alikuwa mtulivu, nakumbuka tukiwa vijana wa miaka 24 tulikwenda wote Roma kusoma Chuo cha Kipapa, tuliporudi tukafanya uchungaji, tukafundisha seminari, kisha tukapelekwa parokiani tukapewa ushemasi,” anasema na kuongeza:
“Julai 6, 1986 tukapata daraja ya upadri, baadaye yeye akawa balozi wa Baba Mtakatifu kwenye nchi tofauti, miaka miwili iliyopita alikuja likizo Tanzania, akaja hapa parokiani ninapokaa, tukafurahi tukala lunch,” amesema.
Amesema siku aliyokuwa arudi New Zealand, alipofika Dar es Salaam aliugua wakampeleka Hospitali ya Kardinali Rugambwa, akatibiwa akapata nafuu na aliweza kusafiri.
“Alipofika New Zealand baada ya kama wiki moja ndipo akapata ugonjwa, alinipigia tukazungumza na akaendelea na matibabu, baadaye wakampeleka Roma ambako alitibiwa na kupata nafuu.
“Mwaka huu, siku ya kumbukumbu yetu ya upadirisho nilimpigia mara mbili hakupokea, jioni nikapiga tena akapokea sista anayeongea Kiswahili ambacho si kizuri akaomba tuongee Kiitaliano, tukazungumza nikwambia nataka kum -wish (kumtakia heri) siku yetu ya upadirisho, akasema baba hajihisi vizuri, nikamuomba amwambie jina langu, akanionyesha video, Askofu Mkuu Rugambwa hakuwa anaweza kuzungumza tena, hadi jana nilipopata taarifa ngumu za kifo chake,” amesema Padri Byamungu.
Akizungumza na Mwananchi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amesema mwili wa Askofu Mkuu Rugambwa unatarajiwa kuzikwa nchini.
“Tunasubiri taarifa rasmi kueleza ni lini mwili wake utaletwa nchini, inawezekana pengine ukazikwa kwenye jimbo lake alikozaliwa. Hata hivyo, wasiliana na Jimbo la Bukoba huenda wao tayari wamepata hiyo tarehe official (rasmi), kwa hapa Tanzania wao ndio wanaotoa taarifa zaidi,” amesema.
Askofu Mwijage wa jimbo hilo, amesema leo Septemba 17, 2025 saa 8:59 mchana hawakuwa wamepata taarifa kutoka Vatican kuhusu taratibu za mazishi.
“Hatujafahamu mwili utakuja lini, utazikwa lini, hatujapata taarifa rasmi za Vatican zaidi ya ile ya kifo chake, hivyo tunaendelea kuwasiliana nao kwa taarifa zaidi kisha tutawajulisha,” amesema.
Wasifu wa Askofu Rugambwa
Askofu Mkuu Novatus Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican, baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadre mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.
Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai mosi, 1991.
Baada ya kufanya kazi mbalimbali katika balozi za Vatican, Juni 28, 2007 Papa Benedikto wa XVI alimteua kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.
Februari 6, 2010, Papa Benedikto XVI, alimteua kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati huo, Machi 18, 2010.
Machi 5, 2015 aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Machi 29, 2019, Papa Francisko alimteua kuwa Balozi wa Vatican nchini New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific.
Machi 30, 2021, Papa Francisko alimwongezea majukumu kwa kumteua kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.
Wakati huohuo aliendelea kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga. Pia Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific.