Auawa kisa ushabiki wa dabi ya Simba, Yanga Songwe

Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamtafuta Evacery Mwaweza mkazi wa Kitongoji cha Ululu kiijiji cha Idiwili kata ya Idiwili wilayani Mbozi mkoani Songwe kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Zabroni Mwambogolo (28) mkazi wa kitongoji hicho wakati wakiangalia mpira wa Simba na Yanga.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Septemba 17,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe,  Augustino Senga amesema   limetokea Septemba 16,2025 saa 12:50 jioni baada ya mabishano ya mpira wa Yanga na Simba.

Kamanda Senga amesema marehemu alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu eneo la kifuani ambapo alifariki dunia wakati anapelekwa katika zahanati ya Iyula iliyopo wilayani humo kwa ajili ya matibabu.

“Uchunguzi wa  tukio hilo umebainika  kuwa ni ushabiki wa mpira wa Simba na Yanga kati ya marehemu na mtuhumiwa. Ambapo mtuhumiwa alitumia kisu alichokuwa nacho wakati wa ugomvi huo kumchoma marehemu kifuani na baada ya kutenda kosa hilo alitoroka kusikojulikana,” amesema Kamanda Senga.

Amesema jeshi hilo linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili akamatwe na aweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.

“Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe linatoa wito Kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kutojihusisha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kusababisha madhara,” amesisitiza kamanda Senga.

Katika tukio lingine Kamanda Senga amesema watu watatu wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha bajaji na gari katika barabara kuu ya Tunduma_Sumbawanga katika kata ya Chipaka Tarafa ya Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.

Kamanda Senga amesema gari aina ya Canter ikiwa inaendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake aligonga bajaji iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina Silasi Malongo (23) mkazi wa Mwaka Tunduma.

Amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 15,2025 saa 3:00 asubuhi ambapo watu watatu waliofariki ni Ibrahimu Kibadeni(16) mwanafunzi, Silasi Malongo(23) dereva bajaji na mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka 30-40 ambaye jina lake halijafahamika aliyefariki akiwa anapatiwa matibabu kituo cha afya Tunduma.

Katika ajali hiyo watu wawili wamejeruhiwa akiwamo Venace Jail (34) na Loyce Kandonga (15) wote wakazi wa Tunduma.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha ni uzembe wa dereva wa gari ambaye aligonga bajaji kwa uzembe wa kutozingatia sheria za usalama barabarani,” amesema Kamanda Senga.