KIUNGO wa zamani Azam FC, Sospeter Bajana ameipa ujanja timu hiyo akisema kwa kikosi ilichonacho kama itazingatia mambo makubwa mawili kutoka kwa kocha Florent Ibenge, basi itafanya maajabu msimu huu.
Bajana aliyeitumikia timu hiyo mfululizo kwa miaka 15, alisitishiwa mkataba wa mwaka mmoja uliosalia Azam wiki chache zilizopita na msimu unaoanza 2025/26 ataichezea JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Bajana aliyekuwa pia nahodha wa Azam, alisema mashabiki wengi wana matarajio makubwa msimu ujao kutokana na uzoefu mkubwa alionao kocha Ibenge, jambo ambalo sio baya, lakini ni lazima wafanye mambo kutimiza ndoto.
Alisema Azam inaweza kuweka rekodi ya kufundishwa na kocha mwenye uzoefu kuliko wote Ligi Kuu Bara, lakini kuna makosa kama yakiendelea mambo yanaweza kujirudia.
“Mimi kwa sasa nabaki kama shabiki wa Azam wa kweli. Niseme tu kocha atakuwa na kazi kama baadhi ya mambo ya muhimu hayatabadilika,” alisema Bajana na kuongeza:
“Jambo la kwanza kubadilisha makocha. Huyu aliyepo sasa anahitaji muda zaidi kusuka kikosi ambacho kitafanya mapinduzi na sio swala la miezi sita au mwaka. Kuna changamoto kubwa ya kubadilisha makocha, unakuta anakuja anakaa msimu mmoja anaondoka, kila mwalimu anafalsafa zake, hivyo haiwezi kuwa rahisi kujenga timu kwa muda mfupi.”
Kuhusu usajili, alisema; “Ishu ya usajili pia ni tatizo, Azam mara nyingi inachukua wachezaji kutoka nje ambao wana viwango vya kawaida, wakija hapa hawana wanachoongeza kwenye timu.”
Ibenge ndiye kocha wa Azam akitoka Al Hilal ya Sudan, ambayo alikuwa akiifundisha msimu uliomalizika na kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa.