OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA. Nicodemus Mkama amesema Tanzania imeweka alama kubwa ya mafanikio katika maendeleo ya masoko ya mitaji huku thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 75.25.
Ongezeko hilo hadi Agosti mwaka huu 2025 imefika Sh.trilioni 55.45 kutoka Sh. trilioni 31.64 Agosti 2021 na mafanikio hayo yametokana na miongozo dhabiti ya kisera, kisheria na kiutendaji inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
CPA.Mkama ameyasema hayo leo Septemba 17,2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hatifungani ya Stawi (Stawi Bond )iliyotolewa na Benki ya TCB ambayo inaweka rekodi ya kuwa hatifungani ya kwanza kutolewa na benki inayomilikiwa na Serikali.


Serikali kupitia CMSA ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
Kuhusu hatifungani ya Stawi amesema anatoa taarifa kwa umma kwamba Stawi Bond imepata idhini ya CMSA ambapo Mamlaka imeidhinisha Waraka wa Matarajio pamoja na nyaraka zingine za mauzo ya Hatifungani hii kwa umma.

“Idhini imetolewa na CMSA baada ya benki ya TCB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani kwa umma”.
Ameongeza kwa mantiki hiyo mauzo ya hatifungani hiyo yamekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya utoaji wa hatifungani kwa umma huku akiipongeza Bodi na Menejimenti ya Benki ya TCB kwa kukidhi matakwa ya kisheria ya utoaji wa hatifungani kwa umma.
CPA.Mkama amesema lengo kuu la Hatifungani hiyo ni kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuziwezesha kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs) kuwa na uwezo wa kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na wakati shughuli za kukuza na kuendeleza biashara.
Pia Utoaji wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

.jpeg)
“Hatifungani hii pia, inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zitakazopatikana zitatumika kuwezesha kampuni za ujasiriamali zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wakati na kwa ufanisi; na wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo kuinua vipato vyao.
“Stawi Bond inaweka rekodi ya kuwa hatifungani ya kwanza kutolewa na benki inayomilikiwa na Serikali. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo uliowekwa kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

.jpeg)
Aidha amesema hatua hiyo inafungua mlango kwa taasisi nyingine za Serikali kuweza kutumia masoko ya mitaji katika kupata fedha za muda mrefu za kugharamia miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
Pia kupitia mauzo ya Hatifungani ya Stawi, Benki ya TCB itaweza kuongeza ukwasi na kuimarisha mtaji na hivyo kuiwezesha benki kutoa huduma kwa makundi mengi zaidi ya wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.
Ameongeza Hatifungani ya Stawi itaimarisha utekelezaji wa mkakati wa Benki ya TCB katika kuongeza ubunifu na hivyo kuimarish utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Naipongeza Serikali kwa kuweka mazingira bora, endelevu na yenye tija kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuinua vipato vyao; na kuwezesha kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs) zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza shughuli za kukuza na kuendeleza biashara kwa wakati na kwa ufanisi.
“Naipongeza Bodi na Uongozi wa Benki ya TCB na wataalam katika masoko ya mitaji waliowezesha kukidhi matakwa ya Sheria, taratibu na Kanuni za Uuzaji wa Hatifungani hii kwa umma.
Pamoja na hayo amesema CMSA itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania (TDV) 2050 yenye lengo la kuwa na uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.