CMSA Yathibitisha Hatifungani ya TCB kwa Umma – Global Publishers

 

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetoa taarifa ya hali ya masoko ya mitaji nchini katika hafla ya uzinduzi wa mauzo ya Hatifungani ya Stawi (Stawi Bond) iliyotolewa na Benki ya TCB, tukio lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Katika taarifa hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA. Nicodemus D. Mkama, alieleza kuwa masoko ya mitaji nchini Tanzania yameendelea kuwa salama, imara, na yanayotoa bidhaa bunifu kwa wawekezaji wa ndani na nje. Tangu Agosti 2021 hadi Agosti 2025, thamani ya uwekezaji katika masoko hayo imeongezeka kwa asilimia 75.25 – kutoka shilingi trilioni 31.64 hadi trilioni 55.45. Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji mzuri wa sera, sheria na miongozo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hatifungani ya Stawi pia imeweka historia kwa kuwa ya kwanza kutolewa na benki inayomilikiwa na Serikali. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo (Alternative Project Financing Strategy), ambao unalenga kusaidia taasisi za umma kupata fedha za miradi ya maendeleo kupitia masoko ya mitaji badala ya kutegemea Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kupitia mauzo ya hatifungani hii, TCB itaongeza ukwasi, kuimarisha mtaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, wajasiriamali na sekta binafsi kwa ujumla. Aidha, benki itaongeza ubunifu wa huduma za kifedha kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko.

Hatifungani ya Stawi imepitia mchakato wa mapitio ya kisheria na kiudhibiti na kupata idhini rasmi ya CMSA. Waraka wa Matarajio na nyaraka nyingine za mauzo ya hatifungani hiyo zimeidhinishwa baada ya TCB kutimiza matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (Sura ya 79) na Miongozo ya mwaka 2019 kuhusu utoaji wa hatifungani kwa umma.

Kupitia hatifungani hiyo, TCB inalenga kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kukuza na kuendeleza biashara zao. Hili ni mojawapo ya malengo ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP) 2020/21–2029/30 pamoja na Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kwa kuwa fedha zitakazopatikana zitaelekezwa kwa kampuni zinazomilikiwa na Watanzania, huku wananchi watakaowekeza wakinufaika kwa kulipwa riba.

CMSA imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza mikakati ya kukuza na kuimarisha masoko ya mitaji kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kwa lengo la kuwa na uchumi jumuishi, shindani na endelevu kwa Watanzania wote.

Katika tukio hilo, CMSA ilikabidhi rasmi idhini ya mauzo ya hatifungani kwa Benki ya TCB, ikiwa ni uthibitisho kuwa bidhaa hiyo ya kifedha imetimiza matakwa ya sheria, kanuni na miongozo ya masoko ya mitaji nchini.