DK.SAMIA ASISITIZA AMANI NA UTULIVU KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29

 Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Unguja 

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amehutubia maelfu ya wananchi wa Mjini Unguja akiendelea na kampeni za kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025 huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza amani na utulivu.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliokusanyika katika uwanja wa Kajengwa, Jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini mkoani Kusini Unguja leo Septemba 17,2025, Dk. Samia amesema utulivu wa kisiasa ni muhimu katika nchi ya Tanzania.

“Tunaingia kipindi cha uchaguzi, mwanzo nilipokuja kujitambulisha ahadi kubwa niliyoitoa ni kuifanya Tanzania iwe yenye amani na utulivu.

“Nilipotembelea kisiwa cha Pemba kubwa waliloniomba wazee wa Pemba ni kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu, hili ndilo ninalotaka nilitilie mkazo,” amesema Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wananchi hao ambako kwake pia ndio nyumbani .

Amesisitiza  wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu aliwaomba wananchi kudumisha amani na utulivu na kufafanua uchaguzi siyo vita bali uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa kupiga kura kisha kurejea nyumbani ili nchi ibaki salama.

“Sasa siyo muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho. Muda wowote kushika silaha iwe ya moto au ya kimila hakuwezi kuleta suluhisho. Ni waombe sana amani na utulivu wa nchi ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine.

Ameongeza: “Nataka niwatoe hofu ndugu zangu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vya Zanzibar vimejipanga vyema kulinda nchi yetu.”

Akifafanua zaidi Dk.Samia amesema “Hutaki kishindo, kapige kura rudi nyumbani tulia. Ni sisitize suala la amani na utulivu.Niwahakikishie vyombo vya ulinzi na usalama viko imara katika kuendelea kulinda amani ya nchi yetu.

Pamoja na hayo Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuwaomba kura wananchi wa Unguja kuhakikisha ikifika Oktoba 29 mwaka huu wanakwenda kupiga kura kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge,Wawakilishi na madiwani wanaotoka na CCM ili waende kuendelea kuleta maendeleo.