Tanga. Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mikanjuni jijini Tanga, Jeremia Mboko amesema msiba uliotokea katika familia ya Francis Kaggi sio msiba wa kawaida ni janga la familia.
Akihubiri kwenye ibada ya maziko iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mikanjuni jijini Tanga leo Jumatano Septemba 17, 2025, Mchungaji Mboko amesema familia kwa sasa haiwezi tena kusema ina sherehe, ila ni msiba mzito kwa familia hiyo.
Mjane Sophia Kaggi akiweka mchanga kwenye kaburi la mume wake, Francis Kaggi wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Kange Kasera jijini Tanga. Picha na Rajabu Athumani
Amesema Alhamisi ya wiki iliyopita alifanya ibada kwenye kanisa hilo kwa ajili ya mazishi ya mama mzazi wa Francis Kaggi na hakuna aliyewaza kwamba na wao wanafuata kwenye safari hiyo.
Hata hivyo, mchungaji huyo amesema aliwaambia waombolezaji kwamba msiba wa bibi yule ni sawa na sherehe kutokana na umri mkubwa aliokuwa nao.
“Nilitaja msiba huo ni sherehe kwa sababu marehemu umri wake ulikuwa ni mkubwa na ndugu walitakiwa kufurahia maisha yake badala ya kulia kwa kuondoka kwake kama mama wa familia hiyo ambaye alikuwa na umri mkubwa,” amesema mchungaji huyo.

Hivyo, Mchungaji Mboka amesema kwa msiba wa familia ya Kaggi, hilo ni janga kubwa na kila mtu mwenye mapenzi mema anapaswa kuiombea familia hiyo akiwamo mkewe kutokana na kuondokewa na ndugu watano kwa muda mmoja.
Kadhalika, Mchungaji Mboko ameipongeza familia ya marehemu Francis kwa kutambua juhudi za kijana ambaye aliwahi eneo la tukio na kusaidia kulinda mali zilizokuwamo kwenye gari sambamba na kuisitiri miili aliyoikuta katika ajali hiyo.

Mjane Sophia Kaggi akiweka shada la maua kwenye kaburi la mtoto wake wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Kange Kasera jijini Tanga. Picha na Rajabu Athumani
“Kwa ulimwengu wa sasa, binadamu wengi wamekosa moyo wa kusaidia hasa kwenye matukio kama haya ya ajali, lakini kijana huyo ameweza hilo kwa kufanikiwa kusaidia waathirika,” amesema mchungaji na kuongeza kuwa:
“Katika kitu ambacho kimenishangaza kwa huyu kijana ni kutunza mali zote ambazo zilikuwa eneo la tukio, ni jambo la ajabu, Miraji hakuwa na tamaa, bali moyo wake ulijaa huruma kwa kuangalia miili na mali husika, hili sio jambo dogo, ni la kupongezwa sana kwa jinsi matukio yanavyotokea.”
Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya familia wakiwa nyumbani kwenye msiba eneo la Magaoni jijini Tanga, kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Chamshama amesema familia inamshukuru sana Miraji Juma kutokana na msaada mkubwa alioutoa wa kuwastili ndugu zao.

Mjane Sophia Kaggi akiweka shada la maua kwenye kaburi la mtoto wake wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Kange Kasera jijini Tanga. Picha na Rajabu Athumani
Amesema Miraji alisimama na kuhakikisha usalama unakuwepo kwa kulinda mali na kutafuta msaada kwa majeruhi sambamba na kuwahifadhi marehemu hadi wananchi wengine walipofika na kutoa msaada zaidi.
“Kutokana na hilo, familia imeamua kumpa heshima maalumu Miraji na kuanzia sasa atakuwa kwenye familia ya Kaggi na huyu sasa ni mwanafamilia wetu,” amesema Chamshama.
Akisoma wasifu wa marehemu wote watano kwa nyakati tofauti kanisani hapo, Chamshama amesema msiba huo ni pigo kubwa kwa familia kwa sababu si jambo la kawaida kuondokewa na kundi kubwa la watu ndani ya muda mchache.

Amemzungumzia pia mdogo marehemu wake kuwa alikuwa mtumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hadi mauti yalipomkuta, ameacha mke na mtoto mmoja aliyemtaja kwa jina la Michelle ambaye ni binti yake wa tatu kuzaliwa kati ya watoto wake wanne.
Amesema Francis alifunga ndoa na Sophia Makange mwaka 2002 na kubahatika kupata watoto wanne ambao watatu kati yao, wamepoteza maisha sambamba na baba yao kwenye ajali hiyo.
Chamshama amesema Janemary ambaye ni binti mkubwa wa marehemu hadi mauti yanamkuta, alikuwa ni Ofisa Biashara na Viwanda, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Mwingine ni binti wa pili wa Francis, Maria aliyehitimu kidato cha sita mwaka huu na kijana wa mwisho, Joshua aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sunrise huku Elineema hadi mauti yanamkuta alikuwa mhasibu wa Tanesco makao makuu.