Dar es Salaam. Wawekezaji katika hatifungani wamepata fursa mpya baada ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB) leo Jumatano Septemba 17, 2025 kuzindua rasmi Hatifungani ya Stawi yenye thamani ya Sh150 bilioni.
Hatifungani hiyo ya miaka mitano inayoashiria kuingia kwa mara ya kwanza kwa TCB katika masoko ya mitaji, inatoa riba ya asilimia 13.5 itakayolipwa kila baada ya robo mwaka. Mapato yatakayopatikana yataelekezwa kwenye mikopo nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) ili kusaidia ukuaji wa biashara na kuongeza ajira.
Kupitia hatua hii, TCB inaungana na taasisi nyingine ambazo hadi sasa zimeorodhesha hatifungani zenye thamani ya jumla ya Sh1.187 trilioni katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo amesema hatifungani hiyo ni zaidi ya chombo cha kifedha.
“Stawi Bond ni uthibitisho wa dhamira ya TCB katika ajenda ya kiuchumi ya Tanzania. Kwa kuwawezesha wajasiriamali na kupanua upatikanaji wa mikopo nafuu, tunahakikisha masoko ya mitaji yanawaletea thamani wahusika halisi wa uchumi wetu,” amesema.
Uzinduzi huo unakuja wakati masoko ya mitaji nchini yanashuhudia ukuaji mkubwa. Kufikia Juni 27, 2025, DSE ilikuwa imefikia mtaji wa jumla wa Sh19.48 trilioni, ukuaji ambao umetokana kwa kiasi kikubwa na sekta za benki na viwanda.
Marekebisho mbalimbali kama kuanzishwa kwa Mahakama ya Masoko ya Mitaji na mabadiliko ya kanuni za DSE yameimarisha uadilifu, ukwasi na ufanisi na hivyo, kuunda mazingira bora kwa bidhaa za kifedha kama Hatifungani ya Stawi.
Viongozi waliohudhuria uzinduzi wa hatifungani hiyo, wamesema hiyo ni hatua muhimu katika kupanua masoko ya mitaji.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya amesema:
“Hatifungani ya Stawi siyo tu chombo cha kifedha cha kuwekeza, bali pia ni njia ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji wa kitaifa, kupunguza utegemezi wa mikopo ya kigeni, na kuongeza mapato ya Serikali.”
Aidha, amesema uamuzi wa Serikali kuunga mkono vyombo hivyo ni muhimu ili kuvifanya vifanikishe malengo yake.
“Uamuzi wenu wa kuwekeza katika Hatifungani ya Stawi si wa kifedha pekee, bali pia ni ishara ya imani kwa benki hii na ajenda ya Serikali ya kuwaunga mkono wajasiriamali,” amewaeleza wawekezaji.
Mwandumbya amesema Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi za fedha kuendeleza bidhaa zaidi za hatifungani kama sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza utegemezi wa mikopo ya gharama kubwa kutoka nje na kuongeza ushiriki wa ndani katika kugharamia maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela ameipongeza TCB kwa safari yake ya mageuzi na kusisitiza kuwa, hatua inayofuata inapaswa kuuza hisa zake kwa wananchi.
“Tangu ilipoanzishwa takribani miaka 100 iliyopita kama Benki ya Posta, TCB imekuwa benki ya wananchi. Kuwawezesha raia kuimiliki kupitia soko la hisa itakuwa hatua ya kihistoria, ikilingana na malengo ya Dira ya 2050 ya kujenga uchumi jumuishi na imara,” amesema.