KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, amesema kutwaa ubingwa wa kwanza na klabu hiyo ndani ya mwezi mmoja tangu kuteuliwa kuinoa ni jambo linalomfanya ajisikie furaha akijivunia mradi wa kujenga kikosi imara kitakachoshindana ndani na nje.
Gamondi aliiongoza Singida juzi Jumatatu kutwaa ubingwa wa mashindano ya Cecafa Kagame, taji ambalo ameliita kuwa mwanzo mzuri wa safari yake na klabu hiyo, huku akifichua mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano mkubwa wa wachezaji wake.
“Kwa kweli najisikia furaha sana. Siku ya kwanza nilipozungumza na rais na viongozi wa klabu hii walinionyesha imani kubwa kwangu na sasa tumefanikiwa kulipa kwa kuwaletea taji la kwanza katika historia ya Singida Black Stars,” alisema Gamondi aliyetwaa tuzo ya Kocha Bora wa michuano hiyo ya 47 iliyoanza Septemba 2-15.
Akiwa na uzoefu mkubwa barani Afrika, Gamondi alieleza kuwa mechi ya fainali dhidi ya Al Hilal ya Sudan haikuwa nyepesi, lakini wachezaji wa timu hiyo walionyesha kiwango bora hasa katika mechi za mwishoni.
“Hakukuwa na kitu rahisi. Tulicheza na timu kubwa, yenye uzoefu na wachezaji bora. Lakini vijana walionyesha ari kubwa na walicheza kana kwamba ni mechi ya Ligi ya Mabingwa. Hilo linanipa moyo na kuamini tunajenga kitu kikubwa hapa,” aliongeza.
Gamondi aliweka wazi kuwa amekuwa akihimiza soka la kushambulia tangu siku ya kwanza na matokeo ya kufunga mabao manne katika mechi mbili zilizopita, nusu dhidi ya KMC (2-0) na fainali dhidi ya Al Hilal (2-1) ni ishara kuwa kikosi hicho kinaanza kuelewa mbinu zake.
“Napenda soka la kushambulia. Napenda kuona timu yangu inafunga mabao. Naamini tumo kwenye njia sahihi, lakini bado tunapaswa kutulia na kuendelea kujifunza. Hatupaswi kuridhika mapema,” alisema.
Kocha huyo pia alimpongeza kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Zambia, Clatous Chama, akisema kiwango chake hakikumshangaza kwa kuwa alimfahamu tangu awali na alijua uwezo wake wa kufanya maamuzi makubwa uwanjani.
“Watu wengi walishangazwa na Chama, lakini mimi sikushangaa. Ni mchezaji mkubwa, na umri si kikwazo. Ni rahisi zaidi kufanya kazi na mchezaji mwenye akili kubwa ya mpira kama yeye,” alisema Gamondi.
Akizungumzia maandalizi ya msimu ujao, Gamondi alisema ubingwa wa Kagame ni chachu ya kujiandaa kwa changamoto mbili kubwa zilizoko mbele yao ambazo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CAF.
“Ni bora kujifunza na kusonga mbele kwa mtindo wa ushindi. Tunahitaji kuendelea kujijenga, lakini kwa kushinda ni rahisi zaidi. Tunatakiwa kuendelea kuimarika kwa ajili ya michuano mikubwa ijayo,” alisema.
Singida Black Stars itasafiri kwenda Rwanda kucheza mechi ya awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports, kabla ya kurejea nchini kuanza kampeni ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26.
Gamondi alisema anaamini kikosi chake sasa kina sura ya ushindani kutokana na usajili wa wachezaji wenye uzoefu na roho ya ushindi, akiwataja Khalid Aucho ambaye ndiye nahodha wa kikosi hicho, Chama na Morice Chukwu kama mifano ya wachezaji wenye “ADN ya ushindi”.