Idadi ya vyoo bora yaongezeka Shinyanga

Shinyanga. Idadi ya vyoo bora imeongezeka mkoani Shinyanga kutoka asilimia 56 hadi 78 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.

Ongezeko la vyoo hivyo limetokana na mradi wa lipa kwa matokeo, hali iliyochangia kupungua kwa mlipuko wa magonjwa ya kuhara.

Akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya lishe na usafi wa mazingira leo Septemba 17, 2025 Ofisa afya Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba amesema kulikuwa na tatizo kubwa la wananchi kutotumia vyoo bora kwenye kaya hali ambayo ilihatarisha afya zao.

“Kupitia mradi huu umewezesha miundombinu kwenye vituo vya afya na zahanati kuimarika kwani vingi vilikuwa havina vyoo bora pamoja na maji, lakini kwa sasa vituo vingi vina huduma zote muhimu vikiwemo vyoo vya kisasa,” amesema Neema.

Amesema hali ilikuwa mbaya kwenye kaya ambapo nyingi zilikuwa hazina vyoo bora na kusababisha wengine kwenda kujisaidia vichakani, lakini kwa sasa mambo yamebadilika taasisi nyingi zikiwemo shule kuna vyoo vyenye ubora pamoja na huduma za maji.

Mkurugenzi wa Shirika la Life Water International Tanzania, Devocatus Kamara amesema wanashirikiana na Serikali kuihamasisha jamii kutumia vyoo bora kwa kuhakikisha vinakuwa na ukuta, paa na sehemu ya kunawia mikono.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akimkabidhi cheti cha pongezi mdau wa usafi wa mazingira Devocatus Kamara

Amesema vyoo vingi vilikuwa havina ubora ambapo baada ya kuingia kwenye jamii waliokuwa wamezingatia utaratibu ilikuwa ni asilimia mbili, lakini kwa sasa vyoo bora vimefikia zaidi ya asilimia 74 kwenye jamii, vijijini ambapo wanashirikiana na kamati za maendeleo za kata na vijiji.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amewataka wakurugenzi kwenda kusimamia suala la usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya chini, na kuunda timu za mabalozi wa mazingira pamoja na kuhakikisha wanahimiza jamii kufanya usafi kuanzia ngazi ya kaya.

Amewataka wakurugenzi kwenda kufanya tathimini ya mitaa misafi na nyumba safi zitambuliwe na kupongezwa, huku wanaokuwa vinara wa uchafu watambuliwe na kuwekwa wazi na kuitaka jamii kuona jukumu la mazingira ni la kila mtu.