Kishapu. Mratibu wa chanjo ya mifugo Wilaya ya Kishapu, John Mchele amesema itafanyika kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo wilayani humo ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mifugo.
Magonjwa yanayolengwa chini ya mpango huo ni homa ya mapafu kwa ng’ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo pamoja na ndui, kideri na mafua kwa kuku.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 17, 2025, katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika kata ya Mwamashele, Kishapu mkoani Shinyanga, Mchele amesema wilaya hiyo imepatiwa dozi 450,000 za chanjo ya homa ya mapafu, dozi 442,000 za sotoka na dozi 300,000 za chanjo ya kuku.
Vilevile, amesema hereni za kielektroniki zimetolewa bure kwa ajili ya utambuzi wa mifugo hiyo.
“Mpango huu utasaidia kupata takwimu sahihi za mifugo na kurahisisha utoaji wa huduma pamoja na kupanga bajeti ya dawa na malisho,” amesema Mchele.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Kishapu, Mwijarubi Mwita amesema hatua hiyo imepunguza tishio la magonjwa ya mifugo na kuongeza mwamko wa wafugaji kushiriki.
“Katika awamu ya kwanza, chanjo ya kuku ilitolewa kwa asilimia 100, huku zoezi zima la chanjo likifikia asilimia 87 ya wafugaji,” amesema Mwita.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amewataka wafugaji kuachana na dhana ya kujivunia idadi kubwa ya mifugo bila faida yoyote kwa familia zao.
“Serikali inataka kuona mifugo inawanufaisha wafugaji kama mtaji wa maendeleo. Watoto wapate elimu bora, familia zipate lishe bora na nyumba bora. Urithi pekee usioharibika ni elimu,” amesema Masindi.
Ameongeza kuwa Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 50 kwa chanjo zote, huku chanjo za kuku na vifaa vya utambuzi vikigawiwa bure.
“Hii itasaidia utambuzi wa idadi halisi ya mifugo, kupunguza wizi, kurahisisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuongeza kipato cha wafugaji kwa sababu mifugo yenye afya huuzwa kwa bei nzuri,” amesema.
Mfugaji Daudi Gamaya kutoka Mwamashele ameishukuru Serikali kwa kutoa chanjo na hereni za mifugo yao, hata hivyo ameiomba iwasaidie dawa za minyoo kwa bei ya ruzuku ili iwe nusu gharama.
Naye mwekezaji na mfugaji wa kata hiyo, Khalidi Hamadi Hilal amesema:
“Kampeni hii ni faida kubwa kwa wafugaji. Tupo tayari kushirikiana kikamilifu ili kuongeza thamani ya mifugo yetu na kupata masoko ya uhakika.