KIGODA CHA MWALIMU NYERERE KUONGOZA KONGAMANO LA UCHUMI JUMUISHI

Zaidi ya wadau 500 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano la Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere litakalofanyika Septemba 18, 2025 kuanzia saa tano asubuhi katika ukumbi wa Nkurumah Lecture Theater, Chuo Kikuu cha Mzumbe – Ndaki ya Mbeya.

Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia katika Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Center).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere, Profesa Alexandra Makuliro, lengo kuu la kongamano ni kujadili uelekeo wa uchumi wa Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya 2050, sambamba na nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukuza uchumi jumuishi.

Wachangia mada wakuu katika kongamano hilo ni pamoja na Bw. David Kafulila (Mkurugenzi wa PPP Center), Dkt. Fred Msemwa (Mkurugenzi wa Tume ya Mipango), Dkt. Gladness Selema (Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki), Dkt. Yasinta Kahyoza (Chuo Kikuu cha Mzumbe), na Dkt. Humphrey Mushi (UDSM).

Mjadala utaongozwa na Mgoda, huku Mwenyekiti wa Kongamano akiwa Profesa Makuliro.