Kila familia ya Gen Z waliofariki Nepal kulipwa Sh42 milioni na Serikali

Serikali ya Nepal imetangaza kutoa rupia 1.5 milioni (Sh42 milioni) kwa ajili ya fidia kwa familia za wafiwa waliofariki katika maandamano ya GenZ yaliotokea nchini humo wiki chache zilizopita.

Fidia hiyo inakuja kufuatia vifo 72 vilivyotokea katika maandamano yaliozuka Septemba 7, 2025 kutokana na marufuku ya mitandao ya kijamii, ufisadi wa baadhi ya viongozi na hali ngumu ya maisha kwa vijana wa taifa hilo.

Imeelezwa kuwa fedha hizo zitagawanywa kupitia Ofisi za Tawala za Wilaya ili kufikia familia za wafiwa ambao wengi walikuwa vijana waliojitokeza kwa wingi katika maandamano yaliokuwa yakipinga ufisadi na hali ngumu ya maisha.

Serikali hiyo pia imetaka uchunguzi wa kina ufanyike juu ya madhara yaliotokea katika machafuko ili kutoa nafasi kwa Serikali hiyo kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na athari hizo na kufanya maboresho kwenye maaeneo yalioharibiwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Om Prakash Aryal amesema ofisi za umma zitapeperushwa bendera nusu mlingoti leo Septemba 17, 2025 ambayo pia ni siku ya maombolezo ya kitaifa kama ishara ya kuwakumbuka waliofariki kwenye maandamano hayo.

Waziri huyo pia ametangaza kuwa serikali imefanya uamuzi wa kuundwa kwa Jengo la Uhamasishaji la Gen Z ili kuwaenzi waliouawa, jambo litakalofanywa kwa kupitia tume iliyoundwa kusimamia jambo hilo.

“Wanafamilia wa waathiriwa, ambao waliuawa katika maandamano ya hivi dhidi ya serikali, watapata fidia kutoka kwa serikali ambayo inaungana nao katika kipindi hiki,”amesema Prakash.

Taifa hilo pia limeruhusu watu kufanya maandamano ya heshima leo Jumatano ili kutoa heshima za mwisho kwa waliofariki.

Maandamano hayo yalianzia katika Hospitali ya Kufundisha ya Chuo Kikuu cha Tribhuvan huko Maharajgunj na kupita mji wa Chabahil na kuishia Pashupati Aryaghat, ambako ibada ya kuchoma maiti imepangwa kufanyika.

Imeandikwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa Mashirika