MSIMU mpya wa 2025-2026 wa Ligi Kuu Bara unaanza leo Jumatano Septemba 17, 2025, huku ukitazamiwa kuongezeka kwa ushindani kutokana na timu 16 shiriki kusajili wachezaji bora wenye uzoefu katika vikosi hivyo.
Wakati ratiba hiyo ikitoka kuashiria kwa msimu wa 2025-2026, Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mechi kali na za kusisimua ambazo kama shabiki au mdau wa soka hupaswi kuzikosa, kutokana na rekodi, ushindani pindi zinapokutana katika Ligi Kuu.
Achana na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16, 2025 kati ya miamba hiyo, lakini pambano la watani wa jadi la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, litapigwa rasmi Desemba 13, 2025, huku Yanga ikiwa ndio mwenyeji.
Mechi ya mkondo wa pili ambayo Simba itakuwa wenyeji itapigwa Aprili 4, 2026, huku miaka ya karibuni Yanga imekuwa na rekodi bora, jambo linalosubiriwa kuona kama pia msimu huu itaendeleza tena ubabe wake, au utavunjwa rasmi. Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga katika Ligi Kuu ilikuwa 2-0, Aprili 16, 2023 na baada ya hapo ilichapwa kwa fedhedha (5-1), Novemba 5, 2023, (2-1), Aprili 20, 2024, (1-0) Oktoba 19, 2024 kisha 2-0, Juni 25, 2025.
Mechi hii ambayo hujulikana kwa jina la ‘Mzizima Derby’ imebeba msisimko kutokana na aina ya ushindani wa nyota wa timu hizo ambapo pambano la kwanza la Ligi Kuu litapigwa Novemba 2, 2025, huku marudiano ni Machi 15, 2026. Simba itakuwa wenyeji wa pambano la kwanza, huku rekodi zikionyesha mara ya mwisho zilipokutana zilitoka sare ya mabao 2-2, Februari 24, 2025, ingawa mechi ya kwanza ya msimu wa 2024-2025 Simba ilishinda 2-0, Septemba 26, 2024.
Hii ni mechi nyingine itakayoleta msisimko wa kuitazama kutokana na aina ya mabenchi ya ufundi na wachezaji wa timu zote mbili, ambapo pambano la kwanza Azam itakuwa mwenyeji Januari 30, 2026, huku ile ya marudiano zikikutana Mei 14, 2026.
Msimu uliopita wa 2024-2025 ziligawana pointi tatu katika mechi mbili ambapo ya kwanza Azam ilishinda 1-0, Novemba 2, 2024, huku ile ya marudiano iliyopigwa Aprili 10, 2025, Yanga iliibuka na ushindi wa 2-1.
SINGIDA BLACK STARS v YANGA
Uwepo wa Kocha, Miguel Gamondi na wachezaji, Khalid Aucho na Clatous Chama katika kikosi cha Singida Black Stars, ambao awali waliitumikia Yanga 2024-2025 ni ishara inayoongeza mvuto zaidi wakati timu hizo zitakapokutana.
Pambano la kwanza kati ya timu hizo mbili litapigwa Februari 23, 2026 na ya marudiano ikichezwa Aprili 15, 2026, huku Yanga ikiwa na rekodi nzuri, baada ya mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilipokutana kwa msimu wa 2024-2025, kushinda zote. Mechi ya kwanza msimu wa 2024-2025, Yanga ilishinda ugenini bao 1-0, Oktoba 30, 2024, huku marudiano ikishinda mabao 2-1, Februari 17, 2025, ikiendeleza pia ubabe kwa kuifunga 2-0, katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), Juni 29, 2025.
SINGIDA BLACK STARS v SIMBA
Hili ni pambano lingine litakalovuta mvuto kwa mashabiki wa soka hapa nchini, ambapo mechi ya kwanza Singida Black Stars itakuwa mwenyeji, Februari 3, 2026, huku ile ya marudiano ambayo itakuwa ni ya mzunguko wa 29, itapigwa, Mei 20, 2026. Msimu uliopita wa 2024-2025, Simba ilishinda mechi mbili za Ligi Kuu Bara, zote bao 1-0, ikianza na ya Desemba 28, 2024 na ya Mei 28, 2025, japo Singida ilishinda mabao 3-1, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), Mei 31, 2025.
AZAM v SINGIDA BLACK STARS
Msimu uliopita wa 2024-2025, timu hizo ziligawana pointi tatu kila moja ambapo pambano la kwanza lililopigwa kwenye Azam Complex, Azam ilishinda mabao 2-1, Novemba 28, 2024, huku marudiano ikichapwa bao 1-0, Aprili 6, 2025. Kwa msimu huu wa 2025-2026, pambano la miamba hii inatazamiwa kuongeza ushindani zaidi kutokana na aina ya wachezaji wa timu zote mbili, ambapo mechi ya kwanza, Azam itakuwa mwenyeji Oktoba 30, 2025, kisha kwenda ugenini Februari 11, 2026.
Hii itakuwa ni mechi nyingine itakayovuta mvuto kwa maafande wa Mashujaa na JKT Tanzania, ambapo pambano la kwanza kwao litakuwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Septemba 18, 2025, huku marudiano yakipigwa Isamuhyo Februari 9, 2026.
Msimu uliopita wa 2024-2025, vita hii ya maafande hakuna aliyeibuka mbabe katika Ligi Kuu Bara, ambapo mechi zote mbili zilitoka suluhu (0-0), ikianza iliyopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Desemba 15, 2024 na ile ya Juni 22, 2025.
TZ PRISONS v JKT TANZANIA
Vita hii ya maafande, itaanza kupigwa Januari 25, 2026, kwa kushuhudia Tanzania Prisons ikiwa ni mwenyeji kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku pambano la marudiano likipigwa kwenye Uwanja Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, Mei 5, 2026.
Msimu uliopita wa 2024-2025, timu hizo kila mmoja ilitamba kwenye uwanja wake, ambapo JKT ilishinda nyumbani kwa bao 1-0, Novemba 24, 2024, huku Prisons ikilipa kisasi katika mechi ya marudiano baada ya kushinda mabao 3-2, Aprili 18, 2025.
MBEYA CITY v TANZANIA PRISONS
Kwa mara nyingine msimu huu wa 2025-2026, itashuhudiwa ‘Derby ya Mbeya’, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo Mbeya City iliyopanda daraja baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, itakuwa na vita kali na maafande wa Tanzania Prisons.
Pambano la kwanza la mechi hiyo litashuhudia Mbeya City ikiwa ndio mwenyeji Oktoba 21, 2025, huku Prisons ikiikaribisha pia kikosi hicho Machi 18, 2026, ikiwa ni ‘Derby’ inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka hususani wa jijini Mbeya.
Msimu wa 2022-2023, ulikuwa wa mwisho kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, ambapo Prisons ilikuwa ndio mbabe baada ya kushinda mabao 2-1, Desemba 25, 2022, raundi ya pili, kufuatia mechi ya kwanza msimu huo kuisha sare ya 1-1, Septemba 9, 2022.